Habari
WIZARA YA HMTH IMEWEZESHA TANZANIA KUWA NA SATELAITI
Na Mwandishi wetu, WHMTH
Kutokana na umuhimu wa uchumi wa teknolojia ya Anga za Juu, serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekaa kikao cha kwanza cha kamati tendaji chenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Teknolojia ya Anga za Juu na Matumizi yake pamoja na umuhimu wake kwa nchi.
Akitoa Maelezo ya Awali kuhusu hali ya matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti katika kikao cha kwanza cha kamati tendaji leo August 2,2023 Jijini Dodoma,Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku amesema Serikali imetoa matamko mbalimbali ili kuiwezesha nchi kuwa mnufaika wa Teknolojia ya Anga za Juu.
Aidha,Munaku amesema Teknolojia ya Anga za Juu ni teknolojia inayotumia uhandisi na sayansi kuchunguza anga za juu za mbali na matumizi yake.
"Teknolojia hii inajumuisha uundaji wa vyombo vya angani, satelaiti, na teknolojia nyingine zinazohusiana Uchumi wa Anga za Juu (Space Economy) unafafanuliwa kwa shughuli zinazotumia rasilimali ya anga za juu kwa ajili ya manufaa ya binadamu na kutokana na umuhimu huu nchi nyingi Duniani zinawekeza katika sayansi na teknolojia ya anga za juu na katika kuendeleza rasilimali watu kwenye sekta hii". amesema Munaku.
Sambamba na Hayo Munaku amesema katika kuwezesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia teknolojia ya anga za juu, Serikali imeunda kamati za Kitaifa (Steering Committee and Technical Committee) kwa lengo la kutimiza azma ya Serikali katika kuimarisha usimamizi, uratibu na uendelezaji wa sekta ya teknolojia ya anga ya juu na kurusha satelaiti nchini.
Ikumbukwe kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi kilichofanyika tarehe 8 Februari, 2022 Dodoma alitamka kuwa “Serikali inafanya jitihada ya kuwa na Satelaiti kwa lengo la kuimarisha mawasiliano.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa Wizara Mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya HMTH, Bw. Mohammed Khamis Abdulla chini ya Mwenyekiti Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu , Sera, Bunge na Uratibu.