Habari
WIZARA YA HABARI NA MAWASILIANO YAJIPANGA KULETA MABADILIKO YA KIJAMII NA KIUCHUMI
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Kamati ya Ukaguzi ya Wizara na mafunzo kwa Kamati hiyo uliofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo CPA, Christopher Nkupama
Dodoma
“Serikali imetupa jukumu kubwa la kuhakikisha Wizara hii inaleta mabadiliko na kuharakisha mapinduzi ya nne ya viwanda na uchumi wa dijitali kupitia Habari na TEHAMA ili tusiachwe nyuma na dunia”, hayo yamezungumzwa na Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akizindua Kamati ya Ukaguzi ya Wizara hiyo jijini Dodoma
Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali imedhamiria kuona TEHAMA inaendelea kuchangia ukuaji wa pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii kwa kuhuisha na kusimamia ipasavyo mifumo ya TEHAMA iliyopo na kuanzisha mifumo mipya ya usimamizi pale itakapoonekana inafaa
Amesema kuwa ni jukumu la kila mtendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha Sekta ya Habari na TEHAMA zinasimamiwa vizuri ili kuwa na mchango chanya wa kujenga, kuimarisha na kustawisha uchumi wa nchi
Dkt. Kijaji ameizungumzia Kamati ya Ukaguzi ya Wizara aliyoizindua rasmi leo tarehe 16 Septemba 2021 kuwa itatekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitatu kuwa itasaidia kushauri kuhusu udhibiti na ukaguzi wa ndani ili kukidhi matarajio yanayotarajiwa kufikiwa kwa wakati na ufanisi mkubwa
Katika hatua nyingine Dkt. Kijaji ametoa rai kwa watendaji walio chini ya Wizara yake kufanya kazi kwa weledi, uzalendo, kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi na kutoa taarifa sahihi kwa umma ili kulinda heshima na hadhi ya nchi ya Tanzania
Akimkaribisha Waziri huyo kuzindua Kamati na Kufungua mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kamati hiyo imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2001 na kanuni zake za mwaka 2004 kama zilivyorekebishwa mwaka 2010 ambapo theluthi mbili ya wajumbe wa kamati hiyo wanatoka nje ya Wizara
Ameongeza kuwa Wizara hiyo haijawahi kupata hati chafu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ambayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo CPA, Christopher Mkupama amekuwa akihudumu katika nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Wizara hiyo
Aidha, amempongeza Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara hiyo CPA, Joyce Christopher kwa ubunifu na utendaji mzuri unaoonesha matokeo
“Wizara hii ni nyeti, wezeshi na mtambuka inayohitaji watendaji wawe na utulivu na usikivu mkubwa ili kuhakikisha malengo tuliyokabidhiwa tunayatimiza kwa kiwango cha juu”, amesema Dkt. Chaula
Dkt. Chaula amesema kuwa Kamati hiyo imepitishwa kwenye utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Anwani za Makazi na Postikodi kwa lengo la kuwashirikisha kwa karibu ili kurahisisha utendaji wao wa kazi na ufuatiliaji kwa kumshauri Afisa masuuli kufanya maamuzi sahihi kwa sababu Kamati hiyo ni jicho la Wizara litakalosaidia kuondosha hoja za ukaguzi
Amesema kuwa katika eneo ambalo Wizara hiyo imefanya vizuri ni eneo la manunuzi ambapo Kitengo cha Manunuzi cha Wizara hiyo kimeweza kusimamia ipasavyo manunuzi na zabuni za Wizara kwa kufuata sheria na taratibu za manunuzi
Kwa Upande wa Mkaguzi wa Ndani Mkuu, CPA Joyce Christopher amesema kuwa lengo la kikao hicho mbali na uzinduzi wa Kamati ya Ukaguzi ya Wizara hiyo ni kuwawezesha wajumbe wa Kamati hiyo kuelewa majukumu yanayotekelezwa chini ya Wizara hiyo ili wanapomshauri Afisa Masuuli wawe na uelewa wa kina wa kile ambacho wanaenda kushauri