Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI YASHIRIKI MAFUNZO YA MFUMO WA NeST-IRINGA


Na Chedaiwe Msuya, WHMTH.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezitaka Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinapeleka watumishi wake kwenye mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST) ili kuboresha usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
 
Hayo yameelezwa leo June 26,2023 na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Mohammed Khamis Abdlulla kwenye Chuo kishiriki cha elimu Mkwawa-Iringa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa NeST yanayoratibiwa na Mamlaka ya usimamizi wa ununuzi wa Umma(PPRA).
 

Amesema PPRA wameweka muda wa miezi mitatu wa kutoa mafunzo kwa taasisi za Umma, na baada ya kipindi cha miezi mitatu ya mpito hakutakuwa tena na mbadala wa kufanya ununuzi wa umma bila kupitia NeST.
 
Licha ya hayo ameeleza kuwa wizara ikiwa ni  mtumiaji wa mfumo huo, imekipa kipaumbele suala hilo na kwamba yeye pamoja na watumishi wake watashirki mafunzo hayo kwa siku zote kama wanafunzi .
 
"Nitahudhuria mafunzo haya kwa siku zote kutokana na ukweli kwamba Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni mdau muhimu wa suala hili kama msimamizi wa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016,"amesema na kuongeza


"Kama mnavyofahamu jukumu la Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi na wadau ni kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanaongezeka lakini pia mifumo hiyo inasoma na ili kuongeza tija na ufanisi ili kukuza uchumi, kulinda rasilimali za Taifa,"anasisitiza
  
Sambamba na hayo Katibu Mkuu ameeleza kuwa kazi ya kujenga mfumo NeST ilianza tarehe 18 Julai 2022, na hadi kufikia leo Juni 2023, Moduli mbili muhimu zimekamilika na kuanza kutumika.
 
Amezitaja moduli hizo kuwa ni ile ya kusimamia usajili wa watumiaji, bidhaa na huduma (e-Registration) na ile ya kuendesha mchakato mzima wa ununuzi kuanzia kuandaa mpango wa mwaka wa ununuzi hadi kumpata mzabuni (e-Tendering).
 
"Kwa hiyo mafunzo haya mnayoshiriki kuanzia leo yatalenga kwenye moduli hizo mbili, Moduli nyingine ikiwemo ile ya kusimamia mikataba ya ununuzi (contract management) , e-Catalogue, e-Auction na e-Payment zinaendelea kujengwa na pindi zitakapokamilika mtaanza kuzitumia,"amesisitiza.
 
Pamoja na hayo ameeleza kuwa,"Kama Serikali mnavyofahamu, Ununuzi wa Umma ni sekta ambayo inachukua kiasi kikubwa cha fedha za Umma hivyo eneo hili la ununuzi wa umma limekuwa likichukua takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali,tunapaswa kulipa kipaumbele,"amesema.
 
Amefafanua kuwa kabla ya kuanza Kwa mfumo wa NeST, Serikali ilikuwa na mfumo wake  wa TANePS ambao umetumika kwa kipindi chote hadi sasa, na umeonesha baadhi ya mafanikio ikiwemo kuongeza usalama wa nyaraka, kupunguza usumbufu wa kutuma zabuni, na kupunguza gharama za mchakato wa ununuzi wa umma.
 
"Mnafahamu kumekuwepo na changamoto mbalimbali Kwenye sekta ya manunuzi hivyo basi Serikali iliamua kutumia teknolojia katika kuendesha na kusimamia ununuzi wa umma ambao ulianza rasmi mnamo Januari 2020,"amefafanua
 
Amebainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, kulionekana kuwepo na changamoto katika matumizi ya TANePS ambayo yaliilazimu Serikali kujenga mfumo mpya.
 
 Mfumo wa NeST unajengwa na wataalam wa hapa nchini, hivyo niwapongeze kwa jitihada hizo na hivyo kama wadau wa matumizi ya Mfumo huo mnayo nafasi ya kuhakikisha mnatoa maoni ya namna bora ya kuboresha mfumo huo na nafasi ipo ya kuendelea kutoa maoni hayo ili kila mmojawetu awe sehemu ya kujenga mfumo.