Habari
WIZARA YA HABARI KUSHIRIKIANA NA INTERNEWS KUZIJENGEA UWEZO JAMII ZA MIPAKANI
Na Chedaiwe Msuya, WHMTH
WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekubali kushirikiana na Shirika la Habari la Internews kuzijengea uwezo wa kuanzisha redio jamii zinazoishi mipakani ili zisiige tamaduni za jamii nyingine nje ya mipaka.
Katibu Mkuu Wizara wa hiyo, Dkt. Jim Yonazi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Bi. Agnes Kayuni, Mkurugenzi wa Internews Tanzania tarehe 13 Desemba 2022 ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma.
"Tunaweza tukasaidiana kuanzisha redio nyingi katika mipaka yetu ambazo zitasaidia wananchi kupata habari hasa za kitaifa na kijamii inayowazunguka. Nchi ya Tanzania ina jamii kubwa zinazoishi mipakani kwa kuwa imepakana na nchi jirani nane hivyo kuna haja ya kuanzisha redio za kijamii katika mipaka yetu," amesema Dkt. Jim Yonazi
Aidha, Dkt. Jim Yonazi amewapongeza Internews kwa kuja na mpango wa kuijengea uwezo jamii kuanzisha redio za kijamii ili taarifa ziwafikie wananchi wa jamii zote hususani wa jamii za pembezoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Internews Tanzania Bi. Agnes Kayuni amesema wameona umuhimu mkubwa wa kuishirikisha Serikali ili walete tija kwa pamoja katika kuwafikia Watanzania.
Ushirikiano huo na Internews Tanzania utahusisha kusambaza habari za ukweli na uhakika kwa wananchi kuhusu Serikali na kuhakikisha kunakuwepo na mawasiliano ya pande zote mbili kati ya Serikali na wananchi.