Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YA HABARI, JWTZ KUSHIRIKIANA SEKTA YA MAWASILIANO


Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdullah ametoa wito kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kuendelea kushirikiana na wizara kwa lengo la kupata uelewa zaidi kuhusu majukumu na miradi inayotekelezwa na wizara.
 
Amesema hayo leo Januari 25, 2024 alipokutana na Kamati ya Wataalam wa Mawasiliano kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania waliofika ofisini kwake kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya mawasiliano.

Bw. Mohammed Khamis Abdullah  ameieleza kamati hiyo iliyooongozwa na Luteni Kanali Lukwaro Mbwambo kuwa wizara kupitia sekta ya mawasiliano ina miradi tisa ambayo inasimamia utekelezaji wake.

Alisema miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa, Mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi, Mradi wa Mfumo wa jamii namba, Mradi wa Usambazaji wa Mawasiliano Vijijini, na Mradi wa Ujenzi wa Data center. 

Aidha, miradi mingine ni Mradi wa Kurusha Satelaiti, Mradi wa Chuo  cha TEHAMA, Mradi wa kuendeleza bunifu katika TEHAMA pamoja na mafunzo kuhusu Teknolojia zinazoibukia katika TEHAMA. 

Akitoa salamu kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Kanali Lukwaro Mbwambo ameishukuru wizara kwa wasilisho hilo na kuahidi kufanya uchambuzi ili kuona ni kwa kiasi gani Jeshi litaweza kutumia miradi hiyo kujiimarisha katika eneo la  mawasiliano. 

Bw. Mohammed Khamis Abdullah ameteua timu ndogo ya Wataalam itayoongozwa na maafisa waandamizi wa wizara ili kuungana na wataalam kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kuja na mapendekezo ya namna ya kuendelea na ushirikiano huu.