Habari
WAZIRI SILAA ASISITIZA UMUHIMU WA ANWANI ZA MAKAZI KATIKA KURAHISISHA UTAMBUZI NA UTOAJI WA HUDUMA

Na Mwandishi Wetu, WMTH Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema kuwa utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi nchini umelenga kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri Silaa ameyasema hayo tarehe 06 Februari, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho ya kwanza ya wiki ya Anwani za Makazi 2025.
Waziri Silaa alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila nyumba, jengo, kiwanja, huduma, ofisi ama eneo la biashara linatambulika kwa Anwani ya Makazi. Anwani ya Makazi inaundwa na Namba ya Anwani maarufu kama namba ya nyumba; Jina la Barabara au Mtaa; na Postikodi.
“ Mfumo wa Anwani za Makazi ni endelevu kwa sababu ya mabadiliko ya makazi, wakazi na huduma, hivyo kufanyika kwa maadhimisho haya kutaongeza hamasa kwa Taasisi za umma na Binafsi pamoja na Wananchi kuweza kutambua na kutumia Anwani za Makazi katika shughuli za kijamii na kiuchumi”, alisisitiza Waziri Silaa
Aliongeza kuwa “Wananchi wana wajibu wa kuzifahamu anwani zao za makazi na kuzitumia katika kujitambulisha, na iwapo watahitaji msaada au ufafanuzi wafike kwa watendaji wa Mitaa, Vijiji ama Shehia au kwa waratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi waliopo katika ofisi za Halmashauri.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange alisema kuwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI ni mdau mkuu katika utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi hususan kupitia kwa watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa ambao wana wajibu wa kuwezesha uwekaji wa miundombinu; kuhuisha taarifa; na kukusanya taarifa mpya.
“TAMISEMI ndiyo yenye wananchi na ndiyo mtoa huduma mkuu kwa wananchi, hivyo TAMISEMI inauhitaji sana Mfumo huu na kwa sasa tulifanya majaribio ya kutoa barua kwa njia ya kidijitali ambapo jambo hilo limeonyesha kuwa la mafanikio,”alisema Mhe. Dkt. Dugange.
Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwa mwaka 2025 yanaadhimishwa kwa mara ya kwanza tangu kukamilika kwa Operesheni Anwani ya Makazi iliyofanyika mwaka 2022 yakiwa na kauli mbiu inayosema “Tambua na Tumia Anwani za Makazi Kurahisisha Utoaji na Upokeaji wa Huduma”.
Maadhimisho haya yanaenda sambamba na maonesho ya Wizara na taasisi zinazotumia Mfumo wa Anwani za Makazi na kilele chake tarehe 8 Februari, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.