Habari
WAZIRI SILAA AITAKA TBC KUAINISHA CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI ZIFANYIWE KAZI
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuainisha changamoto zinazoifanya Redio ya Taifa kutosikika kwa asilimia 100 nchini ili zifanyiwe kazi.
Amesema jukumu la msingi la Shirika la Utangazaji Tanzania ni kuhabarisha umma, hivyo ni muhimu kusikika nchi nzima na kwa kila Mtanzania bila changamoto yoyote.
Waziri Silaa ametoa agizo hilo tarehe 31 Julai, 2024, katika Ofisi za TBC zilizopo Barabara ya Nyerere pamoja na Mikocheni, Dar es Salaam, akiwa katika siku yake ya pili ya ziara ya kuzitembelea taasisi zilizo chini ya Wizara yake.
Akiwa katika ziara hiyo TBC yenye lengo la kufahamu namna vitengo mbalimbali vya shirika hilo vinavyofanya kazi katika kuuhabarisha Umma, Waziri Silaa amepokelewa na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu Dkt. Ayoub Rioba Chacha na kupitishwa katika Historia ya Shirika hilo sambamba na kuona vifaa na Teknolojia zilizotumika zamani na sasa za kurushia matangazo ya redio na Luninga.
Aidha, Waziri Silaa ameitaka TBC kuendeleza maudhui ambayo Taifa linajivunia pamoja na yale yanayoendana na tamaduni za Kitanzania kwa lengo la kuendelea kukuza Ustawi wa Taifa.