Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE KUTEMBELEA ENEO LA TBC, IWAMBI MKOANI MBEYA


Na CHEDAIWE MSUYA, MBEYA

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amemtaka Mkurugenzi wa jiji la Mbeya, Kamati ya Ulinzi na Usalama na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya washirikiane kumaliza mgogoro wa eneo kati ya Shirika la utangazaji TBC na Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ili Shirika la Utangazaji TBC liwekeze katika eneo hilo.

Amewataka kuwatafutia eneo jingine la kujenga Hospitali la Saratani kwani eneo waliloomba limetengwa maalumu kwa ajili ya uwekezaji wa mitambo ya TBC na ukubwa wake ni kulingana na viwango vilivyowekwa na Shirika na Mawasiliano Duniani( International Telecommunications Union, ITU)

Akizungumza katika ziara yake Mkoani Mbeya, Waziri Nape amesema taasisi nyingi za umma hushindwa kumaliza migogoro ya ardhi ambapo matokeo yake migogoro husika inakuwa mikubwa jambo ambalo halipendezi.

"Eneo hili siyo rafiki kwa kuweka Hospitali ya kansa kwani eneo linazungukwa na mionzi,na tunafahamu kuwa mionzi ina madhara makubwa sana, na niwashauri tu mkae mmalize mgogoro huu.  Maelekezo ya Wizara kuhusu eneo hili ni kuwa TBC wapatiwe ili wawekeze kwa maslahi ya Taifa", amesema waziri Nape. 

Aidha, Waziri Nape amesema Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ina eneo lake lenye ekari 25 hivyo wanapaswa kwenda kuwekeza katika eneo hilo ili kupisha migogoro husika.

"Tunapoelekea Kwenye Ripot ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali CAG eneo hili mgogoro usiwepo tena kwa sababu mgogoro huu ni wa muda wa zaidi ya miaka 7, hivyo tuumalize ili shughuli za Kitaifa ziende vizuri", amesisitiza Waziri Nape.

Waziri Nape amesema Mbeya kumekuwa na historia ya kugawiana viwanja juu ya viwanja jambo ambalo siyo sawa ambapo amesisitiza kwa Mkurugenzi wa jiji hilo pamoja na watu wa mipango Miji kumaliza migogoro hiyo.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kufanya ziara zake kwa lengo la kukusanya na kusambaza habari za ukweli na uhakika kuhusu Serikali na Maendeleo ya wananchi na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mawasiliano ya pande zote mbili kati ya Serikali na wananchi.