Habari
WAZIRI NAPE AZINDUA MNARA WA TTCL SINGIDA ,AWAASA WANANCHI KUUTUMIA KWA MAENDELEO YA UCHUMI
Na Chedaiwe Msuya- WHMTH
Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb), amezindua mnara wamawasiliano uliojengwa kwa kusaidiwa na mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano Tanzania TTCL.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo uliofanyika Mkoani Singida ,Wilaya ya Ikungi, Kata ya Misugha, katika viwanja vya shule ya sekondari Dkt. Shein, Mhe. Nnauye amewaasa wananchi kuendelea kuunga mkono Serikali ili kuhakikisha inafanya kazi kwa weledi.
Aidha amewataka wananchi kuwa huduma za mawasiliano zinazopelekwa katika maeneo yao zinatumike kwaajili ya maendeleo na sio kuzitumia kufanya utapeli.
“Wapo wanaotumia huduma hizi kwa kufanya utapeli, niwasisistize wananchi tuchape kazi na kunabaadhi ya maeneo huduma zinatumika vibaya unaona ujumbe unaingia tafadhali tuma kwa namba hii, tunataka hapa huduma hizi zitumike vizuri”, amesema waziri.
Pia kupitia uzinduzi huo Waziri Nnauye amehaidi kuchangia mifuko 400 ya simenti kwaajili ya ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Dkt Shein iliyopo wilayani humo.
Naye Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Peter Selikamba ameiomba kampuni ya mawasiliano Tanzania TTCL kuhakikisha inayapunguzia makampuni fedha ya pango ili kuweza kusaidia hata huduma nyingine zinafika katika eneo hilo kwa urahisi.
Amesema juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan zinaonekana na upambanaji wake wa kupeleka huduma za Umeme, maji na barabara nikwajili ya kuondoa changamoto zilizopo katika jamii.
“Mnapo leta hii miradi ni muhimu kuongea ili tujue ni namna gani mambo yanaweza kwenda,tunatambua mapinduzi mnayoyafanya ni kwaajili ya kupeleka uchumi wetu katika hatua ya kiteknolojia”, amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amesema vijiji sita vinaenda kunufaika, na mnara huo utaenda kuongeza kasi katika biashara na uzalishaji kwa wananchi wa maeneo hayo.
Amesema mfumo huo wa mawasiliano unaenda kubadili mfumo wa kujifunzia katika shule zilizopo katika maeneo hayo ambapo watanufaika na mnara huo uliozinduliwa.
“Tunaomba ndugu zetu wa TTCL mtusaidie kupata huduma ya mtandao ili itusaidia katika shule zetu kuongeza juhudi katika ufundishaji ili kuendana na kasi ya teknolojia ilivyo kwasasa ulimwenguni”, amesema.
Awali Mkurugenzi wa TTCL Muhandisi Peter Ulanga amesema shirika hilo imedhamiria kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya mawasiliano nchini na kuwekeza katika matumizi ya teknolojia.
Aidha ameongeza kwa kusema malengo ya shirika hili nikuwezesha kutoa huduma bora za mawasiliano nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za mawasiliano katika mkoa huo kwa kutumia teknolojia ya 2G, 3G, na 4G hasa katika maeneo ya vijijini.