Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE AZINDUA KAMPENI YA ELIMU KWA UMMA KUHUSU UJENZI WA MINARA 758 YA MAWASILIANO VIJIJINI


Na Mwandishi Wetu

Waziri Nape amezindua kampeni ya elimu kwa umma kuhusu ujenzi wa mradi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini. Hafla hiyo ilifanyika tarehe 24 Januari 2024, katika ukumbi wa jiji, Mjini wa Serikali Mtumba, Dodoma.

Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo, Waziri Nape alieleza kuwa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini ni hatua muhimu kwa kuhakikisha huduma za mawasiliano ya simu (sauti na intaneti/data) zinapatikana kote nchini.

Aidha, ufikishaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali nchini unatarajiwa kuchochea maendeleo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba huduma za mawasiliano ya simu ni nyenzo muhimu katika kukuza shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

Waziri Nape pia alifafanua kuwa, hadi sasa, Serikali kupitia UCSAF imeingia mikataba na watoa Huduma ya Mawasiliano (makampuni ya simu) kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 1,974 zenye vijiji 5,111, kwa ujenzi wa jumla ya minara 2,149. Hii inamaanisha kwamba wananchi takriban 23,798,848 watapata Huduma hiyo ya mawasiliano ya simu kwa uhakika.

Pia, kupitia mradi huu, hadi kufikia mwezi Januari 2024, vibali vyote vya ujenzi vinavyotolewa na NEMC vimekwisha tolewa kwa ajili ya ujenzi wa minara 758. Watoa huduma wamekwisha agiza vifaa, ambavyo tayari vimeanza kuingia nchini. Serikali imeshalipa malipo ya awali kwa wakandarasi wote yenye thamani ya kiasi cha shilingi bilioni 64.5. Ujenzi wa misingi 47 umekamilika, na minara 27 tayari imejengwa, ambapo watoa huduma tayari wameanza kuwasha minara, na kufikia sasa minara 9 imewaka na kuanza kutoa huduma.

Pia, kati ya minara 304 inayopaswa kuongezewa nguvu, ni muhimu kuujulisha umma kuwa jumla ya Minara 190 tayari imeboreshwa na kuongezewa nguvu kutoka teknolojia ya 2G (sauti pekee) kwenda teknolojia ya intaneti/data yaani 3G, 4G.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, viongozi mbalimbali wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), viongozi wa Chama cha Mapinduzi Dodoma, pamoja na wadau mbalimbali wa mawasiliano nchini.