Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE AWASHUKURU WANAHABARI


Na Mwandishi wetu

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amewashukuru Waandishi  Habari wote walioshiriki kuandika habari kuhusiana na maafa yaliyotokea Desemba 3, 2023 katika wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara.

Mhe. Waziri Nape ametoa shukrani hizo leo Januari 19, 2024 alipotembelea wilaya hiyo hususan maeneo ya mji mdogo wa Katesh pamoja na vijiji vya Gendabi na Jorodom ambako kwa kiasi kikubwa kuliathirika na maporomoko ya tope zito zilililoambatana na mawe na magogo, na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi 139 na uharibifu wa mali, nyumba na mashamba.

“Naomba nitoe pongezi za dhati kwa waandishi wa habari wote mlioshiriki kuhanarisha umma wakati maafa. Mmefanya kazi kubwa ya kuchukua taarifa katika mazingira magumu, hivyo tunawashukuru sana”, alishukuru Mhe. Waziri. 

Aidha, amewaomba waandishi wa habari kuendelea kuandika habari kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuirejesha Hanang na maisha ya waathirika katika hali ya kawaida.

Mbali na kuwashukuru waandishi wa habari, Mhe. Nape amewahakikishia wananchi wa Hanang kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Haba ri kwa sasa inachukua juhudi za kuhakikisha  huduma za mawasiliano zinaimarishwa katika wilaya hiyo pamoja na urejeshaji wa miundombinu mingine ikiwemo anuani za makazi.

“Nitoe wito kwa makampuni ya mawasiliano ya simu kuimarisha huduma za mawasiliano ikiwemo kuweka utaratibu mzuri kwa wananchi wa Hanang kupata simu janja hata kwa njia ya mkopo ili waweze kuwasiliana”, ameeleza Mhe. Waziri Nape.

Baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga wakiwa katika Ziara ya Waziri Nape ya kutoa pole na kukagua miundombinu ya mawasiliano, anwani za makazi, na ofisi za posta zilizoathiriwa na mvua, ikisababisha maporomoko ya mawe na tope Hanang Mkoani Manyara, Januari 19, 2024.

 

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Gendabi, Mhe. Daniel Duway ametoa shukrani kwa Serikali kwa juhudi inazoendelea kuzifanya kuwasaidia waathirika wa maafa Hanang.

Naomba niishukuru Serikali na zaidi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kusaida wananchi wetu”, ameeleza Diwani Duway.

Katika ziara hiyo, Waziri Nape aliambatana na mwenyeji wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga, Naibu Katibu Mkuu Bw. Selestine Kakele, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja, Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, Mkurugenzi wa Mawasiliano Bw. Munaku Mulembwa pamoja na viongozi wengine Serikali mkoa wa Manyara na kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.