Habari
WAZIRI NAPE AFUNGUA KIKAO CHA MAWAZIRI WA PAPU
Na Faraja Mpina, WHMTH, Arusha
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amefungua kikao cha Mawaziri wanaohusika na Huduma za Posta kutoka nchi wanachama wa PAPU kilichofanyika Septemba 1, 2023 jijini Arusha.
Kikao hicho kimetumika kama jukwaa la Mawaziri hao kujadili kuhusu maslahi ya pamoja katika sekta ya posta na mashirikiano ya kikanda.
“Majadiliano haya yatatupa fursa ya kujadili namna bora ya kuweka misingi imara ya ustawi wa huduma zetu za posta katika bara la Afrika ili ziendelee kuimarika”, Amesisitiza Waziri Nnauye.
Amesisitiza kuwa kikao hicho ni sehemu ya hafla ya uzinduzi wa Jengo la ofisi za Makao Makuu ya PAPU, ambapo Mawaziri hao wameweza kukaa meza moja kujadili na kubadilishana uzoefu kuhakikisha Huduma za Posta katika nchi za Afrika zinaweza kuendelea kuchangia maendeleo endelevu.
Mawaziri walioshiriki majadiliano hayo ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Kidijiti, Mhe. Mondli Gungubele wa Afrika Kusini, Waziri wa Habari na Elimu ya Uraia, Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashawa wa Malawi, Waziri wa Posta na Mawasiliano ya Simu, Mhe. Worlea Saywah Dunah wa Liberia, Waziri wa TEHAMA na Muongozo wa Kitaifa, Mhe. Dkt. Chris Baryomunsi wa Uganda na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Waziri Nnauye alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Mawaziri na wajumbe wa Mkutano huo kutoka nchi wanachama wa PAPU katika chakula cha jioni usiku wa Septemba mosi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha.