Habari
WATUMISHI WAKUMBUSHWA KUHUSU HAKI NA WAJIBU
a Mwandishi Wetu, Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amelitaka Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo kutumika kuwakumbusha watumishi kuwajibika katika maeneo yao ya kitaaluma.
Akifungua kikao cha Baraza hilo kilichofanyika leo Machi 24, 2023 jijini Dodoma, Bw. Abdulla amesema pamoja na jukumu la Baraza kutetea haki za wafanyakazi bado wanatakiwa kuwajibika katika maeneo yao kwani hakuna haki bila wajibu.
“Baraza ni kiungo muhimu kati ya Menejimenti ya Wizara na wafanyakazi, ni wajibu wetu kufahamu na kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo inayohusu haki, wajibu,stahiki za wafanyakazi na utawala bora”, Amesisitiza Bw. Abdulla
Aidha, Bw. Abdulla amesisitiza wafanyakazi kuwa na upendo, uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na mshikamano ili kutekeleza malengo ya Wizara kwa ufanisi na ofisi yake ipo wazi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amewapongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara na miradi ya maendeleo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; Mfumo wa Anwani za Makazi; na Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Naye, Mwenyekiti wa TUGHE wa Tawi la Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Laurencia Masigo amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kushirikiana na kuombeana mem ana pale patakapokuwa na changamoto yeyote itawasilishwa kwa viongozi ili zitatuliwe.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa BW. Samwel Nyungwa ameipongeza Wizara kwa kufanya vikao vya Baraza kwa wakati na kusisitiza ushirikishwaji wa wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na matukio ya Kitaifa.
Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo kilikuwa mahususi kwa ajili ya kupitia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2022/23 na Makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24.