Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Wataalam wa Sera, Mipango na TEHAMA wapewa elimu kuhusu Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali


 

 

Na Mwandishi Wetu

 

 

Wakurugenzi wa Sera na Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji (DPPs, ADPPs & DMEs) kutoka wizara zote wamepewa elimu kuhusu Mkakati wa Uchumi wa kidigitali wenye lengo la kuboresha mifumo ya TEHAMA katika sekta mbalimbali nchini.

 

Mkakati huo umewasilishwa katika Kikao kazi cha Wakurugenzi wa masuala ya Sera na Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji na TEHAMA kilichofanyika tarehe 23 Februari, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jijini Dodoma.

 

Akifungua Kikao kazi hicho Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa Sera na Mipango, Kamishna wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Bw. Obeid Sayore amesema lengo la kikao hicho ni kupitia Mkakati huo na kujenga uelewa wa pamoja hasa katika kipindi hiki ambacho teknolojia inahamia kwenye ulimwengu wa kidigitali.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw.David Mwankenja amesema TEHAMA inakwenda kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uchumi.

 

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed Mashaka amesema mkakati huo utaleta maendeleo kwa wananchi na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

 

Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mkakati wa Uchumi wa Kidigitali utakaodumu kwa kipindi cha miaka kumi (10) na kusaidia mifumo mbalimbali ya TEHAMA nchini ikiwemo ukusanyi wa mapato.