Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WASHINDI WA SHINDANO LA TEHAMA 2024 KUPITIA HUAWEI TANZANIA KWENDA KUSHINDANA NJE YA NCHI


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye, ametoa rai kwa washindi wanne wa Shindano la TEHAMA 2024 waliochaguliwa kwenda kushindana nchini China kwenye Shindano la kidunia la Huawei ICT Global Competition kwenda kushiriki kikamilifu na kushinda nafasi ya kwanza.

Waziri Nape ametoa rai hiyo baada ya kuwakabidhi washindi tuzo za TEHAMA za Huawei Tanzania kwa mwaka 2024 katika hafla fupi iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mei 10, 2024.

Amesema kuwa mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI hushirikisha wanafunzi wa masomo ya TEHAMA kutoka vyuo vikuu nchini kwa lengo la kutafuta vijana wenye ujuzi katika sekta hiyo ambapo kwa mwaka 2023 washiriki wa Tanzania walishika nafasi ya pili katika shindano la Huawei ICT Global Competition 

“Serikali itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya China katika kuwekeza katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa vijana katika sekta ya TEHAMA ili Tanzania isisalie nyuma katika ukuaji wa teknolojia na mwenendo wa maendeleo duniani”, amesema Waziri Nape.

Amezitaja teknolojia hizo kuwa ni pamoja na Akili Mnemba (Artificial Intelligence) na Intaneti ya Vitu (Internet of Things) na kusisitiza umuhimu wa nchi kuwa na wataalam wenye ujuzi wa teknolojia hizo za kisasa ili kuwezesha kwa mapinduzi nne na ya tano ya viwanda.

Katika hatua nyingine, Waziri Nape alisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya TEHAMA akibainisha kuwa mashindano hayo yamekuwa na ushiriki mdogo wa wanawake, hivyo jitihada zinahitajika ili kuhakikisha usawa na kutoa fursa sawa kwa wanawake katika sekta hiyo.