Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANAWAKE HUATHIRIWA ZAIDI NA MATUMIZI YA MTANDAONI: WAZIRI NAPE


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akikabidhi Tuzo za Kutambuliwa Ushiriki wa Wanawake katika TEHAMA wakati wa Kongamano la Wanawake wa Tanzania Katika TEHAMA (Tanzania Women and Technology Conference) leo Machi 07, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

 

DAR ES SALAAM.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema wanawake ndio huathirika zaidi na matumizi ya mtandaoni ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao.

Waziri Nape ameyasema hayo wakati akifungu Kongamano la Wanawake wa Kitanzania Katika TEHAMA lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), tarehe 07 Machi, 2023, jijini Dar es Salaam.

“Waathirika wakubwa wa unyanyasaji mtandaoni ni wanawake na ndiomana kama Serikali tuna wajibu wa kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivyo”” Amesema Waziri Nape

Waziri Nape ameongeza kuwa Serikali inatunga Sheria ikiwemo ile ya kulinda taarifa binafsi kwa lengo la kuhakikisha anga la mtandao wa Tanzania linakuwa salama ili kuwavutia zaidi wanawake kushiriki katika TEHAMA.

Sambamba na hayo Waziri Nape ametoa rai kwa watumiaji wa mtandao kuwa makini na kuacha kufanya yale yasiyotakiwa katika mtandao ili kujikinga na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya mtandao ikiwemo kukosa ajira mbeleni.

Pia Waziri Nape ameongeza kwa kuwapongeza wanawake kwa kuwa makini kwenye ufanyaji wa shughuli zao, hivyo wakihamasishwa na kushiriki kwa kiwango kikubwa katika TEHAMA basi mapinduzi makubwa ya kiuchumi yatapatikana katika jamii zetu.

Kwa upande wake naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Launch Pad Tanzania, Bi. Carol Ndosi ameiomba Wizara kupitia mamlaka husika kuweza kupitia upya sheria ili ziweze kuwapa uhakika zaidi wa usalama mtandaoni wanawake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika TEHAMA ikiwemo majukwaa ya Kidijitali.