Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANANCHI MOROGORO WAUMWAGIA SIFA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA ANWANI ZA MAKAZI


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Morogoro.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kutoa elimu kuhusu majukumu yake na huduma inazotoa kwa wananchi kupitia sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA kupitia banda la Wizara hiyo lililopo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Mkoani Morogoro yanapofanyika maonesho ya 30 ya Nanenane Kanda ya Mashariki.

Ushiriki wa Wizara katika maonesho hayo umewapatia fursa wananchi wa Morogoro kupata elimu ya Anwani za Makazi na Mfumo wa kielektoniki wa NaPA (National Physical Addressing) unaoonesha utambuzi wa mahali ilipo nyumba, huduma ya kijamii na ilipo ofisi au jengo.

Wananchi wa Morogoro na mikoa mingine waliofika kwenye banda la Wizara na kupata elimu, kwa nyakati tofauti wamepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wizara kwa kutengeneza mfumo huo wa utambuzi kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Kwenye huu mradi wa Anwani za Makazi Wizara imefanya kazi kubwa sana, mnastahili pongezi, mfumo huu wananchi wanauhitaji sana, hasa mfumo wa NaPA, waswahili wanasema mchawi bando tu”, amezungumza Suleiman Mnazi, mkazi wa Morogoro mara baaada ya kupatiwa elimu ya mfumo huo na kuoneshwa mfumo wa NaPA unavyofanya kazi.

Ensinatus Makuwa, mkazi wa Morogoro amesema,”Mfumo huu utanisaidia sana kiutendaji katika kazi yangu ya udereva kwasababu unaonesha mpaka njia ya kupita kufika eneo husika”.

Bwana Makuwa ameonesha imani kubwa na mfumo wa NaPA kwasababu umeandaliwa na wataalamu wa ndani ya nchi, hivyo anaamini utakuwa unaboreshwa mara kwa mara ukilinganisha na taarifa za google Map ambazo haziboreshwi mara kwa mara, akitolea mfano baadhi ya majengo yanabadilishwa majina lakini bado kwenye google map yanasoma majina ya awali.

Mtaalamu wa Mfumo wa NaPA kutoka Wizara hiyo, Bwana Innocent Jacob amesema kuwa, “Wizara imetengeneza programu tumizi ya NaPA (NaPa Application) ili wananchi kupata huduma kwa urahisi. Taarifa zilizopo katika mfumo wa NaPA zinahusisha maeneo yote ya kiutawala, kijamii na makazi ya watu”.

Ameongeza kuwa, Mfumo huo ni endelevu na utaendelea kuboreshwa mara kwa mara ikiwa ni pamoja na zoezi la uhakiki; ukusanyaji wa taarifa za makazi na kuziingiza katika mfumo wa NaPA ili kuboresha na kuuongezea thamani mfumo huo wa utambuzi.