Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANANCHI LINDENI MIUNDOMBINUYA MAWASILIANO: WAZIRI NAPE


Na Mwandishi wetu, WHMTH.

Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nauye (Mb), amesema Serikali inatumia gharama kubwa katika ujenzi wa minara maeneo mbalimbali nchini hivyo ni wajibu wa wananchi kuitunza na kuilinda ili idumu na kuendelea kutoa huduma za mawasiliano.

Waziri Nape ametoa kauli hiyo tarehe 13 Mei, 2024 wakati akizungumza na wananchi akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.

Akitolea mfano wa mnara huo uliojengwa katika kijiji cha Kinua kilichopo Kata ya Namelock, Kiteto Waziri Nape amesema umegharimu kati ya Sh. 300 milioni hadi 350 milioni, na ni mmoja kati ya minara 758 inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini hivyo ni lazima ilindwe.

Kuhusu umuhimu wa miundombinu hiyo ya huduma za Mawasiliano, Waziri Nape ameeleza kuwa ina manufaa makubwa kwa wakazi wa vijijini kwani inawawezesha kuwasiliana kwa urahisi, kutumia huduma za kifedha, kupata huduma za afya na elimu, na pia kutumia mfumo wa anwani za makazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za mawasiliano kwa kuwa ni muhimu katika maisha ya kila siku na kusisitiza kuwa ni haki ya kila mtu kuzipata.

Aidha, Waziri Nape aliupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa jitihada zake za kuhakikisha maeneo ambayo kampuni za simu hazikufanikiwa kupeleka minara kutokana na sababu za kibiashara, yanafikiwa kwa kufadhili ujenzi wa minara.

Amesema kuwa katika minara 758 iliyopangwa kujengwa mwaka wa fedha unaoishia 2024, kampuni ya Airtel imeongoza kwa kukamilisha miradi mingi zaidi kuliko kampuni nyingine za simu, na hivyo wanastahili pongezi.

"Naipongeza kampuni ya simu ya Airtel kwa kazi nzuri wanayoifanya, serikali ina hisa katika kampuni hii, hivyo ni kampuni ya wananchi, na watumiaji wa kampuni ya Airtel wanatumia kampuni yao," alisema Waziri Nape.