Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAKAGUZI WA NDANI WA WHMTH NA TAASISI ZAKE WAKUTANA DODOMA KUTATHMINI UTENDAJI WAONa Jumaa Wange, WHMTH, DODOMA


Wakaguzi wa ndani wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Taasisi zilizo chini yake, kuanzia tarehe 31 Agosti, 2022 mpaka 2 Septemba, 20022 wamefanya kikao kazi cha kujadili shughuli mbalimbali zinazofanywa na vitengo hivyo kwa ajili ya kuboreha utendaji kazi wao kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
 
Kikao kazi hicho kiliongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara hiyo, CPA. Joyce Christopher ambapo ameelezea ni namna gani wataboresha ushirikiano kati ya Wizara na Taasisi ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao yakikazi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ili kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo.

Sambamba na hilo pia Wakaguzi hao wamepitia pia taarifa za ukaguzi ikiwemo kutathmini hatua za utekelezajizi wa mapendekezo ya ukaguzi ikiwemo zile za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Aidha, wakaguzi hao wamejadili kwa pamoja na kusisitiza kushiriki kikamilifu katika kuandaa vitabu vya hesabu za taasisi zao ili kuhakiki ubora wa hesabu hizo kabla hazijawasilishwa kwa CAG hapo tarehe 30 Septemba, 2022

Kwa upande wake nae Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, CPA. Octavian Barnabas amesema kuwa baada ya kikao hicho watafanya majukumu yao kiuadilifu ili kuhakikisha rasilimali za Serikali zinatumika kikamilifu katika majukumu husika.
 
Baada ya kikao kazi hicho wakaguzi hao walitembelea eneo ambapo ofisi mpya za Wizara zinajengwa na kujionea maendeleo ya ujenzi huo pamoja na kufurahishwa na hatua walipofikia mpaka sasa.