Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAHITIMU WA TAALUMA YA HABARI WATAKIWA KUTEKELEZA MISINGI YA TASNIA YA HABARI


 WAHITIMU wa taaluma ya habari na mawasiliano ya umma wametakiwa kutekeleza sera zinazohusiana na masuala ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari ili kutimiza wajibu wa kupasha habari, kuelimisha, kushauri na hata kuiburudisha jamii kwa weledi na ubora wa hali ya juu

 Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye kwenye kongamano la wahitimu wa taaluma ya habari wa shule kuu ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya chuo kikuu chaDar-es-salaam leo Juni 29, jijini Dar es Salaam

Amesema kuwa kipaumbele cha taaluma hiyo kiwe ni kumfikia kila mwananchi kwa kumpatia habari sahihi na iliyojitosheleza kwa wakati pamoja na kumpatia mwananchi nafasi toshelevu ya kutoa maoni yake na kusikika.

“Kama nilivyoanisha kwenye hotuba ya bajeti ya wizara yetu, tunaenda kuboresha zaidi Sekta ya Habari na TEHAMA ili kila mmoja akitekeleza majukumu yake ipasavyo tutaiwezesha Tanzania kuimarika kushiriki uchumi wa kidijitali yanayowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA na pia kuwa na jamii inayopata taarifa sahihi.” Amesema waziri Nape.

 Aidha,waziri Nape  amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya juhudi kubwa za kufungua fursa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha zaidi tasnia ya Habari katika kuhakikisha unakuwepo uhuru zaidi wa habari na kutoa maoni.

“Serikali kupitia Wizara ninayoisimaamia inaendelea kusisitiza weledi na kufuatwa kwa miongozo, maadili, sheria na taratibu mbalimbali zilizowekwa ili muweze kuendelea kuandaa habari zilizo na viwango kwa maendeleo na maslahi mapana ya nchi yetu” amesema Waziri Nape.

Ameongeza kuwa kama ilivyo kwa taaluma nyingine, taaluma ya habari ina misingi, taratibu na miongozo yake ambayo inapaswa kufuatwa ili kuifanya taaluma hiyo iheshimike na kuwatofautisha wanahabari wenye taaluma na wale wanaodhani wanaweza kuwa wanahabari bila kuwa na taaluma hiyo

Aidha, Waziri Nape amewakumbusha wanahabari hao kuandaa habari zenye utafiti wa kutosha  na kutangaza habari chanya za waafrika, hususani watanzania kama ambavyo Rais Samia alivyoonesha mfano bora kwa kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kupitia  kupitia filamu ya The Royal Tour.

Maadhimisho ya miaka 60 ya chuo kikuu cha Dar es salaam yaliyofanyika leo Juni 29, 2022 yamekwenda na kauli mbiu isemayo ni ‘Warsha Kuhusu Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Ushirikiano wa SJMC na Vyombo vya Habari nchini Tanzania’