Habari
WAHARIRI WAPIGWA MSASA KUIFAHAMU WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya mkutano na wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa ili waifahamu Wizara hiyo, taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo na majukumu yake, mafanikio na matarajio ya kuhakikisha jamii ya kitanzania inapata huduma bora za mawasiliano zinazoenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano huo jijini Dodoma, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Wizara yake imeona umuhimu wa kukaa na wahariri hao kwasababu ni watu muhimu katika kuelimisha na kuhabarisha umma namna Serikali inavyohudumia wananchi wake kupitia Sekta ya Mawasiliano.
Amesema kuwa Wizara hiyo yenye miezi sita tu tangu kuundwa kwake ni Wizara yenye majukumu makubwa ya kuleta mabadiliko ya kidijitali kuelekea mapinduzi ya Nne ya Viwanda kupitia TEHAMA.
“Sasa hivi dunia inaelekea kwenye matumizi ya teknolojia zinazoakisi akili za binadamu “artificial intelligence” katika shughuli za kiuchumi ambapo mashine zitakuwa zinafanya kazi zenyewe, hivyo na sisi kama nchi lazima tujipange ili tupige hatua sambamba na mabadiliko haya ya kiteknolojia”, Alisema Dkt. Ndugulile
Ameongeza kuwa Wizara hiyo ina jukumu la kuandaa mazingira wezeshi kuelekea uchumi wa kidijitali, biashara mtandao, kuweka maunganisho ya kidijitali ndani ya Serikali na katika vituo vinavyotoa huduma za kijamii ili kurahisisha ufikishaji wa huduma kwa wananchi kiganjani bila kupanga foleni.
“Wizara hii sio ya mabando tu, ni Wizara yenye majukumu mengi na mazito ya kuwezesha kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi kwasababu inagusa Sekta zote hadi za usalama wa nchi na nyie wahariri ni watu muhimu ambao mnaisaidia Serikali kutoa taarifa, elimu na hamasa kwa wananchi, hivyo mkiifahamu vizuri Wizara basi tunaamini wananchi watapata taarifa sahihi”, alisema Dkt. Ndugulile
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Wizara ina dhamana ya kufanya maandalizi ya kupokea mabadiliko ya kiteknolojia yanayokuja kwa kasi na kuendelea kushauri namna bora ya kupokea na kuitumia teknolojia iliyopo na itakayokuwa ndani ya soko.
Aidha amewashukuru wahariri hao kwa ushiriki katika Mkutano huo kwa sababu wao wakiifahamu vizuri Wizara wataweza kuufikishia umma taarifa sahihi zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa sababu taarifa zote zinapita katika mikono yao kabla ya kwenda kwa wananchi kupitia vyombo vya habari wanavyohudumu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amewahakikishia wahariri wa vyombo vya habari kuwa yeye na watendaji wa Wizara wako tayari muda wowote kufanya kazi na wahariri hao kwa kuwa wao ni daraja baina ya Serikali na wananchi
Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile ameishukuru uongozi wa Wizara kwa kutambua umuhimu wao na kuwaaalika kwenye mkutano huo na wamejifunza na kufahamu majukumu ya Wizara hii kwa taifa