Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UTEKELEZAJI WA OPERESHENI ANWANI MAKAZI SASA NI ASILIMIA 95


Na Juma Wange, DAR ES SALAAM

Zoezi la utekelezaji wa operseheni ya Mfumo wa Anwani za Makazi sasa umefikia  asilimia 95 toka kutangazwa kwake na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyotoa Tarehe 8 Februari, 2022 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Conversion center ambapo alielekeza kuwa utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ufanyike kwa njia ya Operesheni aliyoiita “Operesheni Anwani za Makazi” chini ya usimamizi wa Wakuu wa Mikoa, na kwamba ukamilike ifikapo Mei, 2022.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakati akikabidhi ripoti ya utekelezaji wa zoezi hilo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa siku ya jumamosi tarehe 18  Juni, 20222 katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

“Awali tulikuwa na lengo la kukusanya taarifa na kutoa Anwani za Makazi 11,582,106. Hata hivyo hadi tarehe 31 Mei, 2022 tuliweza kukusanya taarifa na kutoa Anwani za Makazi 12,385,956 sawa na asilimia 106.94. Kati ya Anwani zilizokusanywa Anwani 12,011,576 zina majengo na 374,380 ni viwanja vitupu. Kati ya Anwani 12,011,576 zenye majengo, Anwani 2,011,095 ambazo ni asilimia 16.74 zimebandikwa vibao vya namba za nyumba na Anwani 5,738,552 ambazo ni asilimia 47.77 zimechorwa kwa rangi mithili ya vibao bila kubandikwa vibao.” Amesema Waziri Nape.

“Operesheni hii imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya manufaa yaliyopatikana ni pamoja na kutoa Anwani 12,385,956 ndani ya miezi mitano (5) kazi ambayo awali ilipangwa kufanyika kwa miaka mitano (5), Kuwa na Mfumo wa Kidijitali wenye taarifa muhimu za wananchi, majengo, viwanja na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika majengo hayo pamoja na kutoa ajira za muda kwa vijana wakusanya taarifa 62,813 na wajasiliamali 8,667. Kwa ujumla utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi umefikia zaidi ya asilimia 95 na kwasababu hiyo tunapata ujasiri” amesema Waziri Nape.

Ameongeza kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi ni mfumo endelevu ambao utatumika katika maisha ya kila siku kwa shughuli za Kijamii na Kiuchumi kwani mfumo huu utakuwa na taarifa za msingi ambazo zinaifungua na kuichochea nchi yetu kuelekea uchumi wa kidigitali.

Sambamba na hayo Waziri nape ameongeza kwa kuwapongeza Viongozi na watumishi wa Wizara pamoja na wataalam wa Mfumo wa kidigitali wa Anwani za Makazi ambao wameutengeneza na wamehakikisha unakuwa imara na unatumika wakati wote wa zoezi hili Pamoja na timu ya uratibu ambayo imepambana kuhakikisha shughuli zote zilizopangwa zinatekelezwa kikamilifu. 

Mfumo wa Anwani za Makazi utakapokamilika utekelezaji wake utasaidia kiurahisi uendeshwaji wa zoezi la Sensa ya Wat una Makazi ifikapo 23 Agosti, 2022 kwa kutambua kiurahisi watu na makazi wanayoishi.