Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UFUATILIAJI NA TATHMINI NYENZO MUHIMU YA UTENDAJI WA MATOKEO


Na Faraja Mpina, WHMTH, Morogoro.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewajengea uwezo wataalam wake katika eneo la Ufuatiliaji na Tathmini ili kuimarisha utendaji wa matokeo kwa Wizara na taasisi zake kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yanayofanyika wiki hii mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara hiyo, Bw. Elisa Mbise amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha miradi ya maendeleo ina uwiano na rasilimali zilizotumika na kuleta tija kwa wananchi.

“Mafunzo haya yamelenga kutathmini utayari wa Wizara katika kufanya Ufuatiliji na Tathmini wa majukumu yake hususan utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikijumuisha kuwawezesha wataalam kuandaa mipango yenye malengo yanayotekelezeka na kupimika”, amebainisha Bw. Mbise

Ameongeza kuwa, wataalam hao watapitishwa katika uandaaji wa viashiria vya upimaji katika hatua zote za mnyororo wa matokeo; kubaini taarifa za msingi; mbinu za ukusanyaji taarifa kwa watekelezaji na wasimamizi wa miradi; na namna ya kuandaa taarifa zitakazowezesha wadau hususan viongozi kufanya maamuzi.

Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu, Bi Neema Kilembe amesema kuwa mfumo madhubuti wa Ufuatiliaji na Tathmini unasaidia kuimarisha na kuboresha utendaji wa Serikali katika kuwezesha utekelezaji wa sera, mipango, mikakati, programu na miradi kwa kuongeza uwajibikaji, uwazi na thamani ya fedha za walipa kodi.