Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UCSAF YASHIRIKI KUWEZESHA MABADILIKO YA KIDIJITI NCHINI


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.
 
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unashiriki kuwezesha mabadiliko ya kidijitali nchini kwa kuwaunganisha wananchi waishio vijijini na huduma za mawasiliano, hivyo kuongeza idadi ya watu waliounganishwa na huduma za mawasiliano ya simu na intaneti.
 
Hayo yamezungumzwa leo Aprili 25, 2024 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) katika hafla ya uzinduzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya UCSAF zilizopo Njedengwa jijini Dodoma zilizozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
 
Waziri Nnauye amesema kuwa UCSAF imewezesha watanzania wengi waishio vijijini na maeneo yasiyo na mvuto kibiashara kwa watoa huduma kuweza kuunganishwa na huduma za mawasiliano kupitia ruzuku inayotolewa na mfuko huo kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano yenye teknolojia kuanzia 2G hadi 5G.
 
“Kazi nzuri inayofanywa na UCSAF imewezesha wananchi wa vijijini ambao hawajafikiwa na huduma za kibenki kuweza kufanya miamala kupitia simu za mkononi lakini pia kuongeza idadi ya watumiaji wa miamala hiyo (Mobile money) kutoka milioni 32 mwaka 2020 mpaka kufikia milioni 53 kwa takwimu za sasa ambapo laini za simu zimeongezeka kutoka milioni 51 mwaka 2022 hadi milioni 72 kwa takwimu za sasa”, ameongeza Waziri Nnauye.
 
Aidha, amewahakikishia watanzania kuwa hakuna atakayeachwa bila kuunganishwa na huduma za mawasiliano ambapo ameuzungumzia mradi wa ujenzi wa minara 758 unaoendelea kutekelezwa na UCSAF kwa kushirikiana na watoa huduma utaweza kuwaunganisha watanzania milioni 8 kwa wakati mmoja.
 
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu na Mbunge wa Same Mashariki, Mhe.Anne Kilango Malecela (Mb) amesema Kamati hiyo inaridhishwa na utendaji wa wizara na UCSAF katika kuhakikisha wananchi wote wanaunganishwa na huduma za mawasiliano.
 
Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa mradi wa jengo la Ofisi za Makao Makuu ya UCSAF amesema ujenzi wa Jengo hilo umegharimu shilingi bilioni 3.8 na lina uwezo wa kuhudumia watumishi zaidi ya 100.