Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UCSAF YAPONGEZWA KUJENGA NA KUHAMIA DODOMA


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa taasisi za umma kujenga na kuhamia katika Makao Makuu ya nchi Dodoma.
 
Akizungumza kabla ya kuzindua rasmi jengo la Ofisi za Makao Makuu ya UCSAF leo Aprili 25, 2024 jijini Dodoma, Dkt. Mpango ameupongeza Mfuko huo kwa kujenga jengo lenye viwango na kuzitaka taasisi za umma zote ambazo hazijahamia Dodoma zihakikishe zinatekeleza maelekezo hayo ya Serikali.
 
Uzinduzi wa jengo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mashirikiano mazuri na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya SMZ katika majukumu yao ya kuwafikishia wananchi huduma bora za mawasiliano na kuzitaka sekta nyingine kuiga mfano huo.
 
“Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano Taifa limepiga hatua katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mawasiliano, wakati Muungano ukiasisiwa mwaka 1964 serikalini kulikuwa na Kompyuta moja tu ICL 1500 na ilikuwa Wizara ya Fedha, Hivi sasa matumizi ya kompyuta na intaneti yamefikia watumiaji milioni 35.8", amesema Dkt. Mpango
 
Dkt. Mpango amezungumzia kuanzishwa kwa UCSAF mwaka 2017 ni utekelezaji wa Katiba ya Nchi Ibara ya 18 (a) na (b) kwa kuwa mawasiliano ni haki kikatiba na ya msingi ya mwanadamu na kuupongeza Mfuko wa UCSAF kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaunganisha watanzania kwa kuwezesha ujenzi wa minara ya mawasiliano na pia kupeleka vifaa vya TEHAMA kwa shule 1,121 za umma.
 
Naye Dkt. Mngereza Mzee Miraji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar amesema kuwa wizara hiyo pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zimekuwa na mashirikiano makubwa ambapo kupitia UCSAF vituo vya TEHAMA 11 vilijengwa Unguja na Pemba ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi, lakini pia minara 47 ya mawasiliano imejengwa hivi karibuni.