Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TUJENGE JAMII ILIYOELIMIKA NA IPO TAYARI KWA MABADILIKO YA TEHAMA- NAIBU KATIBU MKUU WA WHMTH


Na Chedaiwe Msuya, Dar es Salaam

Serikali kupitia wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  imewataka wanawake na wasichana kuwa wabunifu na kuanzisha kampuni pamoja na biashara changa kwa lengo la kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine kupitia ubunifu wa TEHAMA.


Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo oktoba 15, 2023 jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bwn.Selestine Gervas Kakele katika  ufunguzi wa mkutano wa wanawake Kwenye kongamano la saba la Ufunguzi wa TEHAMA Tanzania ambapo Takwimu zinaonyesha kuwa, ni asilimia ndogo za Kampuni changa duniani zinazomilikiwa na wanawake.

"Hatuwezi kufanikiwa kujenga jamii iliyoelimika na iliyotayari kuendelea kujifunza na kufaidika na uchumi wa kidigitali endapo kundi muhimu kama wanawake na vijana watabaki nyuma". Amesema.

Aidha, Kakele amewasisitiza wanawake hao kupaza sauti zao na kupitia sauti hizo kama taifa waweze kujadiliana kuhusu vikwazo vinavyowakabili wanawake na kufanya washindwe kuchangamkia matumizi ya Teknolojia na TEHAMA kwa ujumla katika shughuli zao za kila siku.

"Sisi kama Wizara yenye dhamana ya TEHEMA hapa nchini, tungependa kusikia sauti zenu, mkielezea fursa zilizopo na changamoto za matumizi ya TEHEMA"..Amesema

Tutafurahi kusikia kuhusu mawazo yenu, maoni yenu na matarajio yenu kwa serikali juu ya nini kifanyike ili kuendelea kujenga mazingira mazuri na rafiki kwa wanawake kufikia na kutumia teknolojia zinazoibukia". Amesisitiza.

 Vile vile, Kakele amesema Nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali, inakusudia kupunguza na hatimae kuondoa kabisa pengo baina ya watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali na wasiopata fursa hiyo (digital divide). 

"Nguzo hii inaweka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa ya kupata elimu na mafunzo ya TEHAMA kwa jamii". Amesema

"Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mtu pasipokujali hali yake au sehemu anayotoka anashiriki na kufaidika na uchumi wa kidigitali". Ameongezea.


Serikali imedhamiria  kuweka Mazingira mazuri na rafiki ya kisera na kisheria katika kuvutia na kuchochea ubunifu katika TEHAMA pamoja na kukuza vipaji na kuchangia uanzishwaji wa kampuni changa hususan za wanawake na wasichana.

Esta Mengi ni Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni ya TEHAMA amesema Kongamano hilo ni moja ya hatua kubwa ambayo nchi imeifikia kwa kuweka kipaumbele katika TEHAMA kwa maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TEHAMA Dkt Nkundwe Mwasaga amesema kuwa kongamano hilo linakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo Tumia teknolojia Ibukizi katika mapinduzi ya kidigitali ili kutengeneza kazi na kuleta mafanikio kiuchumi na kijamii’

‘Katika siku ya kesho tarehe 17 kwenye kongamano hili tumeweka TEHAMA kwa vijana ikiwa inaendena na mtazamo wa kidunia katika ujumuishi wa kuyashirikisha makundi mbalimbali ambapo tunajadili mafanikio sambamba na kujifunza nchi za nje wao wamefanyaje kuhakikisha uchumi unakwenda vizuri”amesema Dkt Mwasaga.