Habari
“TTCL MMEAMINIWA NA SERIKALI YA RAIS SAMIA, FANYENI KAZI: WAZIRI NAPE
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amesema kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeaminiwa na Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo kuwataka Wachape kazi kwa bidii.
Amesema Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa umehamishiwa TTCL na pia Kituo Cha Data Cha Taifa (Data Center) kinahamishiwa kwenye Shirika hilo la Mawasiliano la Taifa.
Waziri Nape ameyazungumza hayo wakati wa futari iliyoandaliwa na TTCL Tarehe 12 Aprili, 2023 katika ukumbi wa hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
“Mlikoitoa TTCL toka mmeteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia sio hapa ilipo sasa, mmefanya mageuzi makubwa ndani ya shirika na ndio maana Mhe. Rais ameamua kuhamishia miundombinu ya msingi ya mawasiliano na kuileta kwenu ukiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano lakini na Kituo Cha Data Cha Taifa (DATA Center) ambacho pia kinakuja kwenu", amesema Waziri Nape.
Sambamba na hilo Waziri Nape ameongeza na kutoa rai kwa Viongozi wa TTCL kuwa Serikali na Wananchi wanawaamini na wameweka dhamana nzima ya mawasiliano nchini ipo mikononi mwa TTCL hivyo waendelee kufanya kazi nzuri kila siku na wasirudi nyuma.
Waziri Nape aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Selestine Gervas Kakele Pamoja baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara hiyo.