Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

“TASNIA YA HABARI NI NGUZO MUHIMU KATIKA UKUAJI WA UCHUMI: MHANDISI KUNDO”


Na Juma Wange, Zanzibar

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amesema Tasnia ya Habari ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mila na utamaduni wa wananchi wa Afrika.

Naibu Waziri Kundo ameyasema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) katika Mkutano wa Mashirika ya Umma ya Utangazaji Kusini mwa Afrika (SABA) unaofanyika Oktoba 10, 2023 katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.

“Tasnia ya Habari ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mila na utamaduni wa wananchi wa Afrika. Jitihada za makusudi lazima zifanyike kupitia vyombo vyetu vya Utangazaji vya Umma vyenye jukumu la kuyatekeleza hayo. Niwaombe washiriki wote kuhakikisha kuwa maudhui yanayoandaliwa na vyombo vya habari vya umma yazingatie mtizamo wa kuijengea jamii uwezo wa kujitambua na kujivunia uafrika wao.” Amesema Mhandisi Kundo.

Pia mhandisi Kundo amesema kuwa jitihada za makusudi lazima zifanyike kupitia vyombo vyetu vya Utangazaji vya Umma vyenye jukumu la kuyatekeleza hayo pamoja na kuwaomba washiriki wote kuhakikisha kuwa maudhui yanayoandaliwa na vyombo vya habari vya umma yazingatie mtizamo wa kuijengea jamii uwezo wa kujitambua na kujivunia uafrika wao.

Sambamba na hayo Mhandisi kundo amelipongeza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuandaa mkutano huo unaokutanisha wadau mbalimbali barani Afrika na kujadili masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

“Tukio hili la leo ni kati ya matukio makubwa yanayohusu ukuaji wa teknolojia ya habari nchini ambayo yametekelezwa na Wizara kushirikiana na taasisi zake. 

Tunapokutana katika tukio hili muhimu nitumie fursa hii kumpongeza sana Dkt. Ayub Rioba Chacha, Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika letu la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa kufanikisha Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu mkubwa katika visiwa vyetu vya Zanzibar.”Amesema Mhandisi Kundo

Naibu Waziri Kundo ametoa wito kwa wamiliki wa Vyombo vya Habari wanaoshiriki mkutano huo wahakikishe kwamba masuala yote tutakayojadili yanafanyiwa kazi kwa maendeleo ya nchi zetu za Afrika na kama Wizara ipo tayari muda wote kutoa ushirikiano kwa wageni wote ili malengo ya mkutano yaweze kutimia na hatimaye kuleta tija kwa watu wetu.

Mkutano huo umefunguliwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi utakamilika siku ya tarehe 13 Oktoba, 2023 na unatarajiwa kuja na njia mbalimbali zenye kuboresha zaidi Sekta ya Habari nchini na bara la Afrika kwa ujumla.