Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YASAINI MAKUBALIANO YA KIBIASHARA (MoU) NA POSTA OMAN ILI KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA BIASHARA MTANDAO AFRIKA MASHARIKI      •Ushirikiano na Oman utapanua  wigo wa Biashara Mtandao nchini na duniani kote.
 
      •Tanzania kupitia ushirikiano huu utaifanya kuwa kitovu cha Biashara Mtandao katika ukanda wa Afrika Mashariki.
 
       •Tanzania inaiona Posta Oman (Asyad Group) kama mtoa huduma anayeongoza katika Biashara Mtandao (E commerce) katika ukanda huo na lango la masoko ya kimataifa.

 
Leo tarehe 24 Novemba, 2022 Tanzania kupitia Shirika la Posta Tanzania imesaini makubaliano ya kibiashara na Shirika la Posta Oman (Asyad Group) katika Biashara Mtandao lengo likiwa ni kupanua wigo wa kimataifa wa Biashara Mtandao huku ikiiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha Biashara Mtandao kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
 
Hatua hii inafuatia kusainiana makubaliano ya awali baina ya Taasisi hizi mbili (Shirika la Posta Tanzania na Posta ya Oman) yaliyolenga kukuza biashara za posta kupitia ushirikiano wao. Makubaliano hayo yalitiliwa saini na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo na Postamasta Mkuu wa Posta Oman Bw. Nasser Al Sharji, jijini Dar es Salaam yaliyofanywa Mei, 2022 na kushuhudiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye ambaye ndiye msimamizi wa Wizara yenye dhamana na Posta. 

Hivyo, hatua hii ya pili makubaliano yanalenga kukuza Biashara Mtandao nchini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara mtandao kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
 
Kupitia makubaliano hayo , upembuzi yakinifu sasa utafanywa ili kutoa mwelekeo wa kimkakati wa namna ya utekelezaji wa mradi huo na mikakati ya uwekezaji Tanzania kupitia Shirika la Posta huku ikihusisha kutathmini uwezekano wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara mtandao (E-commerce Hub) kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
 
Akielezea umuhimu wa hatua hii mpya katika ushirikiano wa kimkakati na Posta Oman, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo amesema kuwa,
 
“Shirika la Posta linaendelea kupanua wigo wake wa masoko kwa kuendeleza ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani ikidhamiria kukuza biashara za mipakani na kuongeza wigo wa biashara za mtandao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wanapokuwa mahali popote duniani”. Amesema Mbodo.
 
Kwa mara nyingine tena makubaliano hayo ya kibiashara yaliyotiwa saini leo Muscat, nchini Oman yameshuhudiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye huku makubaliano hayo yakiwekwa sahihi na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo na Postamasta Mkuu wa Posta Oman Nasser Al Sharji.
 
Mhe. Waziri Nape yupo nchini Oman kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya Biashara Mtandao (E-Commerce Logistics) nchini kupitia Shirika la Posta Tanzania
 
Mhe. Nape ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Khadija Hamisi Rajabu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) Mohammed Khamis Abdulla, Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya HMTH, Mhandisi Clarence Ichwekeleza, Mkurugenzi wa Uwekezaji kwa Umma, Lightness Mauki pamoja na Katibu wa Shirika la Posta Tanzania, Erick Maxmillian.
 
Chini ya makubaliano hayo Tanzania inatarajia kuwa na eneo maalum litakalotumika kwa shughuli za Biashara Mtandao sambamba na vitendea kazi vya kisasa ili kurahisisha huduma hiyo nchini. Vilevile Tanzania inatazamiwa kupata soko kubwa la biashara mtandao kutoka Oman, kupitia maduka makubwa duniani ambapo mizigo mingi hususani kwa ukanda wa Afrika mashariki itapitia nchini, hii itaongeza pato la Shirika la Taifa kwa ujumla.
 
Postamasta Mkuu Bw. Mbodo ameahidi kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na Posta Oman ili kuwezesha huduma za Posta kuwafikia wateja wengi zaidi baina ya nchini hizi mbili na duniani kote sambamba na kuunganisha soko la Tanzania na Oman katika huduma za Mtandao.