Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAPIGA HATUA HUDUMA ZA POSTA


Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed amezitaka Nchi wanachama za Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kuwa na jitihada mbalimbali za kuboresha huduma za mawasiliano ikiwa ni pamoja na  kuhakikisha wanazijengea uwezo nchi zao na kufanya maeneo ya mijini na vijijini kuunganishwa  na huduma za mawasiliano.

Akizungumza leo jijini Arusha wakati akifunga Mkutano wa 41 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika, Waziri huyo ametolea mfano namna ambavyo Serikali ya Tanzania kama mwanachama wa PAPU inavyounga mkono jitihada za kuboresha sekta ya mawasiliano barani Afrika.

“Tanzania inatekeleza miradi ya kuboresha huduma hizi za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za posta za kidijitali kwa gharama nafuu. Biashara mtandao imeongeza wigo katika soko la dunia na haya ni mabadiliko makubwa, hii biashara mtandao imetoa fursa kwa mteja kutoka Bara la Afrika kununua bidhaa kwa urahisi zaidi”. Amesema Mhe. Waziri Mohamed.

Aidha, ametoa wito kwa Nchi Wanachama wa PAPU kuhakikisha wanaungana na kusaidiana katika kufikia malengo yao na kamwe mipaka ya nchi zao isiwe kikwazo ili wananchi waweze kunufaika na uwepo na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za posta.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Dkt. Sifundo Chief Moyo amesema kuwa Nchi Wanachama wa PAPU wachukue na kutekeleza  yale yote yaliyojadiliwa na kukubalika katika mkutano huo uliolenga kutumia mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma za posta kwa gharama nafuu sambamba na kuchangia uchumi wa nchi zao.