Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA KUWA KITOVU CHA TEHAMA AFRIKA MASHARIKI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akihutubia wakati wa Jukwaa la Uvumbuzi na Teknolojia lenye azma ya kuwezesha mazingira rafiki kwa vijana na wanawake kusimamia miradi ya uvumbuzi lililofanyika jijini Dar es Salaam February 25, 2022.

*Dkt. Yonazi Afungua Rasmi Jukwaa  la Tatu la Uvumbuzi na Teknolojia

 

*Serikali Kuwapa Kipaumbele Vijana na Wanawake katika Matumizi ya TEHAMA

 

 Na Chedaiwe B. Msuya, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habri Dkt. Jim Yonazi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itahakikisha inalifanya kazi suala la ukuaji wa teknolojia nchini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha TEHAMA Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa hotuba yake katika Jukwaa la tatu la Uvumbuzi na Teknolojia lenye azma ya kuwezesha mazingira rafiki kwa vijana na wanawake kusimamia miradi ya uvumbuzi lililofanyika jijini Dar es Salaam Febuari 25, 2022 Dkt Yonazi amesema, Serikali inatambua umuhimu wa uvumbuzi katika mendeleo ya viwanda nchini na duniani kwa ujumla, hivyo kuna haja kubwa ya kuwa na maarifa yanayoendana na mabadiliko haya.

“Kuna mipango mikakati ya kuifanya Tanzania inakuwa kitovu cha TEHAMA Afrika Mashariki kupitia mradi wa “Digital Tanzania” kwa kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa mazingira rafiki ya ufanyajikazi, maarifa, vitendea kazi na mazingira mazuri kwa ajili ya biashara na furaha kwa wote wanaofanyakazi juu ya maendeleo ya TEHAMA” amesema.

Amesema Serikali imefanya mipango mikakati mingi ya kukuza matumizi ya mitandao ya simu nchini ambapo asilimia 94 ya watanzania wanatumia simu za mikononi na asilimia 66 ni ukubwa wa kijiografia wa matumizi ya mtandao nchi nzima huku watumiaji wa Intaneti wakiongezeka kutoka milioni 5 kwa mwaka 2010 hadi kufikia milioni 29.8 mwezi Disemba 2021.

“licha ya namba ya watumiaji wa intaneti kuongezeka kutoka Milioni 5 kwa mwaka 2010 hadi Milioni 29.8 Disemba 2021, tunaamini kuwa bado haitoshi kutokana na uhitaji mkubwa wa upatikanaji wa huduma hii kwa watu wa maeneo ya vijijini na kuwafanya watu wafurahie uwepo wa intaneti, ila kikubwa ni kuhakikisha vijana wanakuwa mstari wa mbele katika matumizi ya mtandao juu ya shughuli zao mbalimbali” amesema.

Amesema, Serikali inafanya jitihada kubwa kuwekeza katika TEHAMA, na inatambua kuwa nguvu kazi kubwa ni vijana, wanatakiwa kuhakikisha wanajipa changamoto za kimaendeleo binafsi kutokana na fursa mbalimbali zinazopatikana kutokana na matumizi mazuri ya TEHAMA ili kuleta maendeleo nchini na kuinua maisha yao binafsi.

Ameongezea kuwa, Serikali ina jukumu kubwa kuhakikisha nchi inaendana sawa na ukuaji wa sekta ya Mawasiliano, Uvumbuzi, na maarifa kwa kuwapa kipau mbele wanawake.

Amesema, mapinduzi ya kidijitali yanakua kwa kasi nchini na uwekezaji mkubwa umefanyika kama utungaji wa sera ya mwaka 2016, upanuaji wigo wa usalama wa mtandao, na muunganiko wa matumizi ya mtandao maeneo ya vijijini ambapo Wizara imetoa jukumu kwa Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Wizarani, Mulembwa Mnaku kuhakikisha azma ya Serikali kuifanya TEHAMA inakuwa uti wa mgongo wa Taifa katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Sambamba na hilo, Dkt Yonazi amewakaribisha wadau mbalimbali kutoa michango yao juu ya mbinu za kukuza sekta ya TEHAMA, na kuahidi kuwa kwa mara nyingine tena, mdahalo na jukwaa hilo litafanyika kisayansi ziadi kwa kuwalika watunga sheria, wadau wa viwanda na wanataaluma.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka amesema, Serikali inaendelea kufanya mabadiliko ya Mtaala wa Elimu hususani katika ngazi ya vyuo vikuu nchini kuhakikisha wanatoa masomo yanayowajengea vijana maarifa na uzoefu wa hali halisi ya maisha baada ya kumaliza chuo, ili kuhakikisha vijana wanajijengea uwezo wa kujiajiri.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Bi. Christine Musisi amesema, UNDP inatarajia kuendeleza mjadala huo wa TEHAMA nchini nzima ili kufikisha elimu zaidi kwa watanzania wote.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Amos Nungu amesema wakati akifungua jukwaa la tatu Uvumbuzi na Teknolojia lenye lengo la kuwezesha mazingira rafiki kwa vijana na wanawake kuongoza miradi ya uvumbuzi kuwa, kuna umuhimu mkubwa kwa watanzania hususani vijana na wanawake kuhakikisha wanatunza Teknolojia na kuwa endelevu na COSTECH kama moja ya wadau wakubwa katika ukuaji wa teknolojia nchini, watafanyia kazi michango mbalimbali itakayotolewa katika kongamano hilo.