Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

“TANZANIA IKO KWENYE RELI KUHAKIKISHA INTANETI YA MWENDOKASI INAFIKIA WANANCHI WENGI ZAIDI” MHE. NAPE MOSES NNAUYE


Na Mwandishi Wetu Geneva, Uswiss, Julai 11,2023
 
Mhe. Nape Moses Nnauye amesema kuwa Tanzania iko kwenye reli kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wanapata mawasiliano ya intaneti ya mwendokasi na yenye tija kwa wote nchini.
 
Mheshimiwa Nape ameyasema hayo jijini Geneva leo kwenye Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU Council ambayo Tanzania ni Mjumbe baada ya kuchaguliwa mwaka jana kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Januari mwaka huu.
 
“Naamini kuwa, mada ya “Kuhakikisha Mawasiliano ya intaneti ya kasi na yenye tija kwa wote: Je tupo kwenye reli?” imekuja katika wakati muafaka. Swali tunalojiuliza ni “Je tupo kwenye reli?” aliuliza Mhe. Nape Nauye

“Naomba nianze kwa kusema kwamba “Ingawa bado hatujafika kule tunakokusudia kwenda, lakini hatupo kule tulipokuwa”. Alifafanua Mhe. Nnauye. Aidha alisema kwa Tanzania hatua ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha uwepo wa mtandao wa Intaneti ya kasi kila mahali Tanzania. Na akaongeza kuwa hatua inayofuatia ilikuwa ni kusogea kutoka kwenye dhana ya mtandao kila mahali kwenda kwenye dhana ya mtandao kwa kila mtu.

Hivyo basi, hivi sasa tunahitaji kuangalia matumizi ya intaneti ya kasi na yenye tija kwa kila mtu.  Naamini kwamba, mtandao wa Intaneti ya kasi na yenye tija lazima uwawezeshe watumiaji kufanya shughuli mtandaoni kwa gharama nafuu, kwa usalama, na kwa ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.

Amesema pia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa Intaneti ya kasi (broadband coverage) kwa zaidi ya asilimia 80 ya maeneo wanayoishi watu wake. Hata hivyo amesema kuwa ipo idadi kubwa ya wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo ambayo yana mtandao wa 3G, 4G na hata 5G, lakini bado hawanufaiki kwa kiasi kikubwa na huduma za kidijitali zinazowezeshwa na mtandao wa intaneti ya kasi kutokana na gharama kubwa ya simu janja, upatikanaji wa maudhui ya ndani, bei ya huduma za data, na kukosekana kwa elimu ya kutumia huduma za kidijitali.

 

Hali kadhalika, Mheshimiwa Nape ameuambia Mkutano huo kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kutekeleza programu za kuwajengea wananchi uelewa juu ya matumizi ya huduma za kidijiti, kupunguza ada kwa uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano (Right of ways) na kuondoa tozo katika huduma za mawasiliano ili kuongeza unafuu wa huduma.

Mheshimiwa Nape pia amesema Serikali imeondoa tozo katika huduma za pesa mtandao kwa kuzingatia kuwa Watanzania wengi wanatumia huduma za kifedha kupitia kwenye simu zao (Mobile Money), na kwa kuzingatia kuwa matumizi ya pesa mtandao ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa kidigiti na kuongeza ufanisi wa matumizi ya TEHAMA.  

Pia Serikali imeendelea na kuwahimiza watoa huduma za mawasiliano pamoja na zile za kifedha, kuweka utaratibu wa kuwakopesha au kuwapatia wateja wao simu janja kwa masharti nafuu.

Akimalizia hotuba yake Mheshimiwa Nape aliuambia Mkutano huu kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa intaneti ya kasi na yenye tija ndio msingi wa mafanikio ya mageuzi ya kidigitali. Aidha alitoa wito wa kuendeleza mashirikiano na wadau wa kimataifa na kikanda katika kuimarisha na kuhakikisha kwamba lengo la kuwa na Inatenti ya Kasi na yenye tija linafikiwa kwa kila Mtu.
 
Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano maalum wa ITU unaojadili masuala ya “Metaverse” utakaofanyika tarehe 12 Septemba 2023 na utafuatiwa na Kongamano lenye mada ya “Miji na Metaverse: matumizi ya Metaverse kwa wote” litakalofanyika tarehe 13 Septemba 2023. Tanzania pia inatarajiwa kuwa pia mwenyeji wa mkutano wa ITU-T wa Kundi Kazi la 20 unaojadili masuala ya Intaneti ya Vitu (Intanet of Things) na Miji na Jamii Endelevu kuanzia tarehe 13 had 22 Septemba 2023, katika Jiji la Arusha.