Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SHIRIKA LA POSTA LAAZIMIA KUTOA HUDUMA BORA NA SALAMA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema Shirika la Posta linatakiwa kubuni mikakati inayoendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya Teknolojia na Mawasiliano Duniani ili huduma zake zikidhi mabadiliko hayo kwa ubora na usalama.
 
Bw. Mohammed Khamis Abdulla ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya Umoja wa Posta Duniani Juu ya Usalama wa Huduma za Kiposta kwa Nchi za Afrika iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha tarehe 28 Septemba, 2022.
 
“Mafunzo haya yanatoa nafasi kubadilisha uzoefu, kujadiliana na kubuni mbinu na mikakati ya kuhakikisha huduma za kiposta nchini zinakuwa zenye viwango vya juu na usalama ili kujenga uaminifu zaidi kwa wateja wanaotumia huduma za Posta,” amesema Abdulla. 

Ameongeza kuwa mafunzo hayo imebidi yatolewe kutokana na  na Dunia ya sasa inahitaji huduma za uhakika na zenye usalama ili kuendana na Teknolojia ya Mawasiliano. 
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Bw. Sifundo Chief Moyo, alieleza kufurahishwa na Warsha hiyo na kupongeza Tanzania kwa kutambua umuhimu wa kuboresha huduma za mawasiliano ya kiposta. 

“Usalama wa huduma za posta ni moja ya njia kuu katika kudumisha mahusiano na nchi zetu za Afrika na Dunia kwa ujumla,” aliongeza. 
 
Warsha hiyo imeandaliwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) na inatarajiwa kufanyika kwa siku 3 jijini Arusha kuanzia tarehe 28-30 Septemba 2022.