Habari
SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI KUKUZA SEKTA YA HABARI
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema mabadiliko yaliyofanyika ya Sheria za Huduma za Habari yataenda kukuza Sekta ya Habari kwa kiwango kikubwa.
Mhe. Nape Moses Nnauye ameyasema hayo baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha mabadiliko hayo ya Sheria hiyo, Bungeni, jijini Dodoma, leo Juni 13, 2023.
“Mabadiliko yaliyofanyika yataenda kukuza Sekta yetu ya Habari kwa kiwango kikubwa sana. Yataongeza uhuru wa kujieleza, haki na wajibu lakini pia yatakwenda kushughulikia tatizo kubwa la hadhi ya Wanahabari ambayo ni kuifanya kazi ya Habari iwe taaluma na ikiwa taaluma itakuwa na kipato ambacho kinaelezeka kwa mujibu wa Sheria”- amesema Waziri Nape.
Katika hatua nyingine Waziri Nape amesema Katika Sheria hiyo kumeondolewa jinai ambapo ni jambo zuri na litajenga Tasnia ya Habari ikue na kuendelea vizuri.
Sambamba na hayo Waziri Nape amempongeza Mkuu wa Nchi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ndiye aliyeagiza mapitio ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kumshukuru kwa uamuzi wake huo mzuri.
Waziri Nape ameziomba taasisi za kimataifa ambazo zinafanya tathmini ya hali ya demokrasia, Uhuru wa Wanahabari na Uhuru wa Kujieleza, zitumie taarifa za sasa hivi baada ya mabadiliko haya kufanya tathmini. Maana wamekuwa wakitumia taarifa za muda mrefu na kuifanya nchi kuonekana kama haijapiga hatua wakati Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mengi katika kurekebisha uhuru wa watu kujieleza, uhuru wa Wanahabari na kupanua wigo wa demokrasia.