Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAPONGEZWA UJENZI WA CHUO CHA TEHAMA


Na Juma Wange

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa uamuzi wake wa kuanza ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA jijini, Dodoma. 

Pongezi hizo zimetolewa na Mhe. Mhandisi Mwanaisha Ulenge (Mb) wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo tarehe 05 Februari, 2024.

"Hivi karibuni tumeshuhudia serikali imeingia makubaliano na wadau wale ambao wanatusaidia kuona kwamba chuo hiki cha TEHAMA kinakwenda kukamilika,”  amesema Mhe. Ulenge. 

Mhe. Mhandisi Ulenge ameendelea kutoa pongezi kwa serikali kwa kufanya jambo kubwa kwa vijana wa Kitanzania kupitia ujenzi wa chuo hicho. 

Amesema kuwa, chuo hicho si kama vyuo vingine vinavyofundisha ICT au masuala mengine ya shahada ya Teknolojia ya Habari bali chuo hicho kinakwenda kuondoa pengo lililokuwepo katika masuala ya Teknolojia. 

Ametoa wito kwa vyuo vingine nchini kukiunga mkono chuo hicho ili kuondoa ombwe lililokuwepo kwa vyuo vingine vya KITEHAMA nchini.