Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAFANYA MAGEUZI MAKUBWA SHIRIKA LA TTCL


Waziri wa Habari, MMawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 23 nchini baina ya TTCL na HUAWEI Tanzania leo Aprili 17 2023 jijini Dodoma.Kushoto wanaosaini mkataba ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa HUAWEI Tanzania Bw. Damon Zhang

 

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mageuzi makubwa katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuhamishia shughuli zote za miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Shirika hilo.

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amezungumza hayo leo Aprili 17, 2023 jijini Dodoma akiwa mgeni rasmi katika hafla ya utiaji saini mkataba wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 23 nchini baina ya TTCL na Kampuni ya HUAWEI Tanzania.

 

Waziri Nape ameyazungumzia mageuzi hayo kwa lengo la kuboresha utendaji wa TTCL ni pamoja na Rais Samia kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuanzia ngazi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika na Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja toka uteuzi wao Shirika limepiga hatua.

 

Ameongeza kuwa changamoto nyingi za TTCL ni za kihistoria, akitolea mfano taarifa ya ukaguzi ya mwaka 2017/18  iliyoonesha  jumla ya shilingi Bilioni 91.43 kama madeni yasiyo na vielelezo. Tatizo lilionekana kuanzia taarifa za hesabu za mwaka 2009 ikiwa ni miaka mingi kabla ya Serikali kurudishiwa umiliki wa Kampuni ya Simu Tanzania.

 

Amebainisha kuwa tatizo la mahesabu ya TTCL lilianza toka Shirika likiwa la ubia kabla ya kurudishwa Serikalini kwa asilimia 100 na moja ya sababu za Serikali kuvunja ubia ilikuwa ni kutofautiana kwa taarifa za hesabu.

Kuhusu madeni yasiyo na vielelezo na yasiyoweza kukusanywa ya jumla ya shilingi bilioni 7.51 yaliyoonekana katika ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2021/22, amesema tayari yamefanyiwa kazi na kubainika kuwa wateja wanadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 5.7 hivyo kupunguza hoja hiyo kutoka bilioni 7.51 mpaka bilioni 1.8.

 

Aidha, Waziri Nape ametoa rai kwa TTCL kuhakikisha kuwa inafanyia kazi maelekezo ya Mhe. Rais kwa Shirika kuangalia maeneo ya kupunguza gharama na kuwekeza kwenye maeneo ambayo itaweza kufanya vizuri zaidi na kuzalisha faida.

 

“Rais ana imani na TTCL hasa baada ya mageuzi makubwa yaliyofanyika ya usafishaji wa hesabu za Shirika; kufuta madeni ya zamani na kuondoa mali zilizokaa muda mrefu bila kutumika. Tunataka TTCL liwe Shirika la mfano barani Afrika kwa kutimiza ndoto za kuanzishwa kwake”, amesisitiza Waziri Nape.