Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAELEKEZWA KUWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KUKABILIANA NA UHALIFU WA KIMTANDAO


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma

Serikali imeelekezwa kuhakikisha kuwa inaweka mikakati madhubuti ya kushirikisha kampuni za simu katika kukabiliana na uhalifu wa kimtandao.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb), tarehe 03 Februari, 2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati hiyo kuanzia Februari 2024 hadi Januari 2025.  

Mhe. Kakoso amesema kuwa suala la utapeli na uhalifu mwingine wa kimtandao bado linajitokeza nchini. Na kusisitiza kuwa jambo hili, linalotokana na maendeleo ya TEHAMA, linahatarisha uchumi na jamii na linahitaji ufumbuzi wa kina.

Akisoma maazimio ya Kamati ya Bunge, Mhe. Kakoso ameitaka Serikali iimarishe udhibiti wa uhuru wa mitandao kwa kuzingatia umuhimu wa demokrasia yenye mipaka. 

Mhe. Kakoso ameitaka Serikali kuhakikisha TCRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaweka mikakati madhubuti inayohusisha kampuni za simu kukabiliana na uhalifu wa kimtandao. Na kuongeza kuwa 

Serikali ihakikishe kwamba makampuni ya simu yanawajibika ipasavyo na kutoa nafuu za kisheria kwa waathirika wa uhalifu wa kimtandao. Na kwamba hatua hizi zinakusudiwa kuboresha udhibiti na usimamizi wa mitandao ili kupunguza uhalifu wa kimtandao na kusaidia waathirika kupata msaada wa kisheria.