Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUPELEKA WATUMISHI NJE KUJIFUNZA TEKNOLOJIA YA AKILI MNEMBA


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amesema Serikali imechukua jitihada za kutosha kujenga uwezo kwa wataalamu na kuandaa miongozo ya kisera na kisheria ambayo itatalinda na kuchochea matumizi sahihi na salama ya Teknolojia zinazoibukia ikiwemo Akili Mnemba. 

Naibu Waziri kundo ameyasema hayo akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Nape Nnauye (Mb), leo Februari 08, 2024, Bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mpendae, Mhe. Toufiq Turky (Mb).

“Kwa sasa, tayari Serikali imetoa ufadhili wa masomo ya muda mrefu na muda mfupi kwa watumishi wa umma 500 kwenye maeneo ya Teknolojia zinazoibukia ikiwemo eneo la matumizi ya akili mnemba. Kati ya watumishi 500, watumishi 20 tayari wameanza masomo ya kozi ya muda mrefu na nafasi 480 zilizobaki tayari Serikali imetangaza nafasi hizo na mchakato wa kupokea maombi unaendelea.” amesema Mhandisi Kundo

Pia, Wizara imeanza taratibu za ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA kitakachojengwa Nala, Dodoma kwa lengo la kuzalisha wataalam watakaokidhi mahitaji yaliyopo kwa sasa likiwemo hitaji la Akili Mnemba. Ujenzi wa chuo hiki unaenda sambamba na ujenzi wa Vituo vya ubunifu nane (8) kwenye maeneo ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeya, Arusha, Lindi, na Zanzibar. Aidha, Wizara imeboresha Sera ya TEHAMA ya mwaka, 2016 kwa kuandaa rasimu mpya ya Sera ya mwaka 2024 ambayo inajumuisha maeneo ya Akili Mnemba.

Sambamba na hilo, Wizara imekamilisha Mkakati wa miaka kumi (10) wa Uchumi wa kidijitali unaoainisha maeneo muhimu ya matumizi ya Akili Mnemba katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Kidijitali.