Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUJUMUISHA ANUAI ZA JAMII KWENYE TEHAMA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Jim Yonazi akizungumza wakati akifunga kikao cha wadau cha kujumjuisha anuai za jamaii katika TEHAMA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Ndege leo tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma

 

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kiuhakikisha kuwa anuai za jamii zinajumuishwa kwenye TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro wakati akifungua kikao cha wadau wa taasisi za Serikali na anuai za jamii ikiwemo watu wenye ulemavu, vijana, wazee na wanawake ili kuhakikisha kuwa anuai hizo za jamii zinajumuishwa kwenye TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili makundi hayo maalum yaweze kutumia na kunufaika na TEHAMA nchini. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Ndege, Dodoma.

Dkt. Ndumbaro amesema kutokana na mabadiliko ya TEHAMA duniani ambapo imepelekea huduma nyingi kutolewa kupitia TEHAMA, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itahakikisha kuwa huduma hizi zinatolewa na kumfikia kila mwanachi kwa wakati ili kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 kwa kutambua na kukusanya mahitaji ya anuai za jamii ili yajumuishwe kwenye TEHAMA.

 

Ameongeza kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2026 kwa lengo la kuboresha na kukuza maunganisho ya ndani na ya kimataifa ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa huduma mbali mbali za Serikali kwa wananchi kidijitali.

“Lengo la Mradi huu ni kuboresha na kukuza maunganisho ya ndani na ya kimataifa ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa wananchi kwa kujenga vituo vya ubunifu vya TEHAMA ili kuboresha ubunifu kwa kupitia na kuhuisha sera na sheria mbalimbali ili kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji na uendelezaji wa Sekta ya Mawasiliano pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa TEHAMA nchini” amesema Dkt. Ndumbaro.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Ernest Kimaya ameishukuru Serikali kwa kuwaalika na ameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza vifaa rafiki vya TEHAMA na matumizi yake kwa wananchi hususani kwa anuai za jamii ikiwa ni pamoja na kushirikisha watendaji wa anuai za jamii katika ngazi za kata hadi taifa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI itumike kufikisha na kutekeleza hili

Akizungumza kuwakilisha kundi la wajasiriamali nchini, Mwenyekiti wa Wamachinga wa Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi amesema kuwa mradi wa Tanzania ya Kidijitali ni chachu kwao kwa kuwa utarahisisha shughuli zao na kuwawezesha kufanya biashara mtandao kwa kuwa wana umoja unaowaunganisha wamachinga wote na kusajiliwa kwenye kanzi data ambayo inarahisisha mawasiliano baina yao na Serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakati akifunga kikao hicho amesema kuwa mabadiliko ya teknolojia yanagusa maisha yetu ya kila siku katika nyanja za kiuchumi na kijamii ambapo Serikali kwa kutambua hili imeweka sera, sheria, kanuni pamoja na kujenga miundombinu ya TEHAMA, kutoa huduma za mawasiliano ili kuhakikisha kuwa wananchi wote pamoja na anuai za jamii zinajumuishwa na kushirikishwa katika TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali

“Kila mmoja wetu atekeleze maazimio mliyokubaliana kwa kuwa taifa hili halina mtu mwingine wa kuliendeleza ila sisi ili taifa letu liweze kuwa mbele na kunufaika na TEHAMA,” amesisitiza Dkt. Yonazi

Naye Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka wazee na kuwajumuisha kwa kuwa wakizungumza katika jamii sauti zao zinasikika kwa kuwa wapo wazee wenye nguvu, utaalamu na hawawezi kuwa nje ya mabadiliko ya teknolojia

Akitoa wasilisho kuhusu mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Jumanne Makumbato amesema kuwa mradi huu umejikita katika maeneo matatu ambayo ni ikolojia ya kidijitali itakayohusisha kuweka mazingira wezeshaji na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA; maunganisho ya kidijitali ambayo itajikita kwenye upatikanaji wa mawasiliano ndani ya Serikali na kufikisha mawasiliano yenye kasi vijijini kwa maendeleo ya wananchi; pamoja na jukwaa la huduma za kidijitali ambapo eneo hili litahusika na mifumo, huduma, miundombinu ya kuhifadhi data, kujenga uelewa na uwezo wa wananchi katika masuala ya kidijitali