Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUIMARISHA MAWASILIANO YA SIMU WILAYA YA MKOANI KUSINI PEMBA


Serikali imeahidi kwenda kufanya tathmini ili kubaini maeneo yenye changamoto ya mawasiliano katika Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba na hatimaye kumaliza kabisa changamoto hiyo.

Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Maryam Azan Mwinyi kuhusu changamoto ya mawasiliano katika eneo hilo.

“Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia UCSAF ilijenga minara miwili chini ya Zantel katika Kata za Kengeja na Mgagadu, na katika Kata ya Mtangani mnara ulijengwa na Kampuni ya simu ya Halotel,” amefafanua Mhandisi Mahundi.

“Mheshimiwa Spika, Serikali itakwenda tena kufanya tathmini ili kujua maeneo yaliyobaki yenye changamoto na kuona iwapo minara hiyo itahitajika kuongezwa nguvu au kama kuna uhitaji wa ujenzi wa minara mipya na utekelezwaji utafanyika kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha,“ amesema Mhandisi Mahundi.

Katika swali lake Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itayaunganisha maeneo yenye changamoto ya Mawasiliano ya Simu katika Mkoa wa Kusini Pemba kwenye Mkongo wa Taifa ili kuondoa kabisa tatizo hilo.