Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUHAMASISHA WANAHABARI WA AFRIKA KULINDA BARA LAO


Na Mwandishi Wetu - WHMTH,

Serikali imesema katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari kwa Bara la Afrika yatakayofanyika nchini Ghana, Tanzania inakwenda na msimamo wa kuhamasisha waandishi wa habari wa bara hilo kulinda na kutetea Bara lao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), tarehe 03 Aprili, 2024 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambako Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ( Mb) alikuwa mgeni rasmi.

"Maadhimisho haya yanafanyika duniani, na katika Bara la Afrika tutakuwa na maadhimisho makubwa Ghana na sisi kama Tanzania tuna ushiriki wetu na msimamo wetu wa kuwahamasisha waandishi wa habari wa Bara la Afrika kulinda na kulitetea Bara lao lakini na kuhakikisha watawala katika bara hili wanasimamia rasilimali za bara hili ili zinufaishe bara letu", alisema Waziri Nape.

Mhe. Nape alisema wana habari wana nguvu katika kuhamasisha jambo wakitaka na ushahidi ulionekana wakati wa Corona, kwa kampeni kubwa iliyopigwa na wanahabari mpaka vijijini kwani ilisaidia kuokoa maisha ya watu wengi waliofahamu umuhimu wa kunawa mikono, kuchukua hatua na mambo mengine ya kujikinga na janga lile.

Waziri Nape alisema ni matumaini yake kwamba hata kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inayosema "Jukumu la Wanahabari katika kulinda sayari ya Dunia, na hasa katikati ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na hali ya mazingira", itafanyika kampeni kubwa kuhakikisha wanaokoa mazingira na kuifanya dunia kuwa eneo salama.