Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SEKTA YA POSTA KUIKOMBOA AFRIKA KIUCHUMI


Na Faraja Mpina, WHMTH, Arusha

Waziri wa Habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amesema kuimarisha huduma za posta katika Bara la Afrika kunaweza kulikomboa bara hilo kiuchumi na kuchochea maendeleo.

“Kama kupitia Posta tuliwezesha ukombozi wa Bara la Afrika kisiasa, kupitia Posta tunaweza kuwezesha ukombozi wa Bara la Afrika kiuchumi. Dhamira ipo, uwezo upo, mazingira yana ruhusu na sababu za kufanya hivyo zipo”

Waziri Nnauye ameyazungumza hayo jijini Arusha katika halfla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) uliofanywa leo tarehe 2 septemba 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 Ameongeza kuwa kushikamana kwa bara la Afrika ni njia sahihi ya kujikomboa kiuchumi na umoja wa posta upo tayari kuwezesha kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo.

“Sekta ya posta huwezesha shughuli za biashara, kijamii na kiuchumi miongoni mwa mataifa ya Afrika kupitia majukwaa ya kidijitali huku ikithibitisha jukumu lake la uwezeshaji wa uchumi wa kidijitali”, amesema Waziri Nnauye.

Aidha, ameizungumzia hafla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya PAPU kuwa kilele cha Kikao cha 41 cha Baraza la Utawala la PAPU kilichofanyika jijini Arusha ambacho kilijadili na kuhamasisha mabadiliko ya Sekta ya Posta Afrika ili kuimarisha uchumi wa kisasa wa kidijitali. 

Naye Katibu Mkuu wa PAPU, Bw. Sifundo Chief Moyo amesema imefika hatua sasa ya Sekta ya Posta Afrika kuwa sekta muhimu katika kuchangia mabadiliko ya kidijitali katika jamii. Amelizungumzia jengo la PAPU kuwa kituo cha mabadiliko ya kidijitali na uratibu wa maendeleo ya sekta ya posta katika bara la Afrika