Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SEKTA YA POSTA HUIONGEZEA THAMANI BIASHARA MTANDAO, ASEMA NAPE


Na Faraja Mpina, WHMTH, Arusha

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa rai kwa nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika kuzingatia mabadiliko ya mazingira ya Kimataifa ya utandawazi na mapinduzi ya teknolojia ya TEHAMA ili kutoa huduma bora za posta zenye kuaminika na zenye faida kwa biashara ndogo ndogo na za kati.

Waziri Nnauye ameyasema hayo wakati akifungua jukwaa la wasimamizi na watoa huduma za posta kutoka ndani na nje ya bara la Afrika lililofanyika leo Agosti 31 jijini Arusha ambapo ameizungumzia Sekta ya posta kuwa inaongeza thamani mlolongo mzima wa ufanyikaji wa biashara kwa njia ya mtandao.

“Jukumu letu kama wasimamizi, watoa huduma na washirika wa sekta ya posta ni kujitahidi kuwa na usawa wa mifumo ya usimamizi na uwezo wa utoaji wa huduma za posta ndani ya bara letu la Afrika licha ya utofauti wa Serikali zetu katika usimamizi wa sekta hii”, amesema Waziri Nnauye.

Ameongeza kuwa, kama bara la Afrika tunatakiwa kuendelea kutumia mikutano hii kuimarisha ushirikiano ambao utatoa suluhisho la masuala mbalimbali ya sekta ya posta ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha Ofisi zetu za Posta za nchi za Afrika ili ziweze kufungua fursa za kijamii na kiuchumi kwa kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma za posta barani Afrika.

“Tumekuwa tukizungumzia "Afrika Moja, Bara Moja, Posta Moja" lakini, shughuli za huduma za posta hutofautiana kutoka nchi moja ya Afrika hadi nyingine, hivyo mikutano kama hii itumike kuweka usawa katika utungaji wa Sera, uendeshaji, udhibiti na utoaji wa huduma za posta katika bara la Afrika.

Amebainisha kuwa, mtandao wa posta barani Afrika una mchango mkubwa katika kutoa huduma muhimu kwa maendeleo ya kila siku, miundombinu ya posta inatumika kuziba pengo la kidijitali hasa maeneo ya vijijini, kupitia utoaji wa huduma mbalimbali za TEHAMA ambapo kwa Tanzania, Shirika la Posta lina vituo vya TEHAMA 36 vinavyotoa huduma ya intaneti vilivyopo katika ofisi sita za posta.

Naye, Postamasta wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo amesema kuwa mkutano huo unatumika kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za pamoja wanazokutana nazo kama Afrika katika sekta ya posta na namna ya kuzitatua ili kufanya taasisi na mashirika ya posta kufanya vizuri zaidi na kusaidia maendeleo ya nchi zote za Umoja wa Afrika.

“Kama nchi tumepiga hatua, posta ya sasa sio ile ya barua tu, leo tunazungumzia posta ambayo ni zaidi ya barua, leo unaweza kununua chochote unachokitaka kupitia kwenye duka letu mtandao na tukachukua na kukupelekea popote ndani na nje ya nchi”, Amesema Mbodo.