Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SAFARI CHANELI KUTUMIKA KUTANGAZA UTALII NA SEKTA ZA UCHUMI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati kikao cha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi kuhusu uendeshaji wa Televisheni ya Safari Channeli kilichofanyika leo Mei 30, 2022 jijini Dodoma.

DODOMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutanua wigo wa kujitangaza ndani na nje ya nchi ili kuendelea kufungua fursa mbalimbali za uchumi kupitia sekta ya utalii na Sekta nyingine za uchumi ambapo televisheni ya Safari Chaneli imeonekana kuwa ni nyenzo muhimu sana kwa ajili ya kutangaza utalii na kuitangaza nchi na fursa mbalimbali zinazopatikana nchini

Akizungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi kuhusu uendeshaji wa Chaneli ya Safari kilichofanyika leo Mei 30, 2022 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi ametoa wito kwa sekta za umma kutumia channeli hiyo kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana nchini

“Nitoe wito kwa Sekta za Umma nchini kutumia Safari Chaneli kutangaza sekta zao kwa mtazamo wa utalii tukiwa wabunifu kila sekta ya uchumi inaweza kuwa sehemu ya utalii,

kuna fursa katika usafirishaji, mawasiliano, kilimo ambapo watu wanaweza kujifunza nchini kwetu kupitia chaneli hii ya utalii”, amezungumza Dkt. Yonazi

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. John Jingu amesema kuwa Serikali na wadau kutoka sekta binafsi wanalo jukumu la kuhakikisha wanawekeza kwa kiasi kikubwa katika Chaneli hiyo ya Safari ili malengo ya kukuza utalii kupitia channel hiyo na watu wengi ndani na nje ya nchi waweze kufahamu vivutio vilivyopo nchini yaweze kufanikiwa

“Tunahitaji kuongeza jitihada za uwekezaji wa rasilimali katika chaneli hii  ya Safari hasa rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji, rasilimali hizo zitatolewa na wadau ambao ni taasisi za umma lakini pia sekta binafsi ambao ni wadau wa utalii nao wanapaswa pia kuwekeza kadri watakavyoona manufaa yanayopatikana kupitia chaneli hiyo kuwekeza ili kukuza sekta ya utalii nchini”, amezungumza Dkt. Jingu

Kwa upande wa Bi Fatma Hamad Rajab, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amesema kuwa Zanzibar ni kituo kikubwa cha utalii na tayari ipo safari chaneli kupitia ZBC 3, ambapo ameahidi kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na Tanzania Bara kwa ubunifu mkubwa ili kupitia ZBC 3 milango mingi zaidi ya utalii itafunguka

Kwa upande wa Meneja Uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bi Martha Chassama amesema kuwa TFS imepata mafanikio makubwa sana katika kutangaza maeneo yao ya utalii kupitia Safari Chaneli  na imekwishatoa kiasi cha fedha kuchangia uendeshaji wa Chanel hiyo ili kuendelea kujitangaza na kuonekana zaidi ndani na nje ya nchi

Akizungumza katika kikao hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) dkt. Ayub Rioba amesema kupitia Safari Chaneli watanzania wanazidi kujua na kulinda uhifadhi, inaonesha umuhimu na kuhamasisha utalii wa ndani lakini pia dunia inatambua vivutio vingi vya utalii vinavyopatikana nchini