Habari
RAIS SAMIA ARIDHIA KUONDOLEWA TOZO ZA MIAMALA YA SIMU
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuondolewa kwa tozo za miamala ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu za mikononi.
Hayo yamesemwa Julai 3, 2023 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa kwa lengo ya kukagua uhakiki na uhamasishaji wa anwani za makazi pamoja na kukagua minara ya mawasiliano inayojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mkoani humo.
“Rais Samia ameridhia ombi hilo lililopelekwa na Waziri wa Wizara yetu ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) ambalo lilikuwa ni kilio cha Watanzania”.
Ameongeza kusema Rais Samia ameona fahari ya yeye kuwa Rais ni kuwasikiliza wananchi anaowaongoza na ndio maana ameruhusu ombi hilo.