Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

POSTA YAJIVUNIA MTANDAO MPANA WA KUFANYA BIASHARA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema Shirika la Posta Tanzania (TPC) lipo katika mkakati wa kujiingiza zaidi katika biashara mtandao kwa sababu Shirika hilo lina faida ya kuwa na mtandao mpana ndani ya nchi na kuunganishwa na matawi mbalimbali ya posta yaliyopo katika nchi  nyingine.

 

Dkt. Ndugulile amezungumza hayo alipotembelewa ofisini kwake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) Younouss Djibrine kwa ajili ya kufahamiana na kuzungumzia taarifa za mafanikio na kubadilishana mawazo kuhusu huduma za posta katika bara la Afrika.

 

Aliongeza kuwa kuna mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za posta nchini ambapo kwa sasa Shirika hilo limejikita kwenye usafirishaji wa vifurushi na vipeto, biashara ya kubadilisha fedha na biashara mtandao.

 

“Tunataka kujiingiza zaidi katika biashara mtandao kwasababu tuna faida ya kuwa na mtandao mkubwa  wa matawi mengi ya Shirika hili ndani ya nchi na kuunganishwa na ya nchi nyingine na huduma hii imekwishaanza kufanyika”, Dkt. Ndugulile

 

Amesema kuwa wamedhamiria kuboresha huduma za posta kuanzia muonekano wa majengo, matumizi ya mifumo ya TEHAMA, kubadilisha muonekano na tabia za wafanyakazi ili wateja wa Shirika hilo wapate huduma bora kwa wakati.

 

“Tumeendelea kudhibiti na kuimarisha mifumo yetu, vifurushi vyote vinakaguliwa ili kuhakikisha kwamba vinakuwa salama kusafirisha ndani ya nchi na hata nchi za nje”, Dkt Ndugulile

 

Naye Katibu Mkuu PAPU, Younouss Djibrine amesema kuwa huduma za posta zimeweza kutambuliwa duniani kuwa ni moja ya huduma muhimu hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Korona ambapo Shirika hilo limekuwa likifikisha vifurushi hadi mlangoni, kutoa huduma za kifedha na sasa limeanza kuwa kituo cha kutoa huduma jumuishi

 

Amesema kuwa Shirika la Posta lina matawi zaidi ya 650,000 duniani kote yaliyounganishwa pamoja hivyo inakuwa rahisi kwa Shirika hilo kufanya biashara mtandao na kufikisha huduma katika maeneo mbalimbali duniani.

 

Aidha, ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao inautoa kwa PAPU katika kipindi hiki na kusema kauli ya ‘Hapa kazi tu’ inaakisi juhudi kubwa ya Serikali ya Tanzania kwa Umoja huo.

 

Sote tunafahamu kuwa Ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika zinajengwa katika jiji la Arusha katika barabara ya Moshi- Namanga, jengo ambalo linatarajiwa kuwa jengo refu kuliko yote katika jiji hilo na linatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Machi 2022.