Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

POSTA MUWE KINARA UTEKELEZAJI WA ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI NCHI NZIMA


  • Anwani za Makazi ni Msingi wa Posta ya Kidijitali

 

Prisca Ulomi na Loema Joseph, Dodoma

Serikali imelielekeza Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuwa kinara na kuongoza jukumu la utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi linaloendelea nchi nzima

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye wakati akifungua rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma leo

Waziri Nape amesema kuwa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi utafanikisha na kuwezesha Posta ya Kidijitali na utendaji wa Shirika katika kuhudumia wateja na wananchi kwa ujumla na amewataka Mameneja wote wa TPC kushiriki kikamilifu katika jambo hili la anwani za makazi

“Mameneja wa Mikoa yote wa Shirika la Posta Tanzania muwe wajumbe maalum na wa kudumu kwenye kamati ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima na muongoze utekelezaji wa jambo hili mikoa yote nchi nzima”, amesititiza Waziri Nape

Amewataka wajumbe wa Baraza la 28 la Mkutano huo kujadili kwa uwazi, kuambizana ukweli na kukosoana kwa staha ili kujenga umoja, kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika kwa kuwa anatambua kuwa uhai wa Shirika umebebwa na wafanyakazi wenyewe na Wizara itawasiliana na Wizara ya Fedha ya Mipango ili kufanikisha malipo ya deni la shilingi bilioni 26 kwa lengo la kuliondolea mzigo Shirika

Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Nape, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa wateja wanataka kuona TPC ya kisasa inayofanana na mashirika mengine duniani na tayari TPC imeonesha taswira hii na Shirika linakua kiuchumi

“Wateja wetu cha kwanza anachokutana nacho siyo huduma unayompatia bali unavyompokea na kumhudumia, hivyo tuhudumie wateja wetu vizuri, tuipeleke mbele Serikali kwa kuwa tunawakilisha Serikali na tunafanya kazi kwa niaba ya Serikali,” amesisitiza Dkt. Yonazi  

Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa TPC, Macrice Mbodo amesema kuwa katika mkutano huo, wajumbe watapatiwa mafunzo ya huduma kwa mteja; kupitia Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (2022/33 – 2025/26) unaojikita kuifanya Posta ya Kidijitali kwa maendeleo endelevu; na kupitia bajeti na majukumu ya Shirika hilo kwa mwaka 2022/23

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wengine, Meneja wa TPC wa Mkoa wa Dodoma, Ferdinand Kabyemela amemshukuru Waziri Nape kwa kuwatengeneza, wataishi kwa upendo ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika kwa kuwa wana rubani na kapteni mzuri Mbodo anayewaongoza vema kutekeleza majukumu ya Shirika

Pia, mkutano huo umehudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalum (Wafanyakazi), Mhe. Dkt. Alice Karungi Kaijage; Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Justina Mashiba; na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Samson Mwela