Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NDUGULILE AJIKITA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAWASILIANO YA SIMU NA DATA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake inashirikiana na wadau wa sekta ya mawasiliano kuhakikisha inatatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili wananchi waweze kupata huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu katika maeneo yote nchini.

 

Amezungumza hayo katika kikao chake cha majadiliano na Watendaji Wakuu wa makampuni ya simu Tanzania kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma kwa lengo la kutatua changamoto na kuwa na mkakati wa pamoja wa kuongeza wigo wa mawasiliano ya kasi ya simu na data nchini.

 

Ndugulile amesema kuwa matamanio ya Serikali ni wananchi wake kuweza kutumia mawasiliano ya simu na data kufanya biashara mtandao, kupata huduma mbalimbali za Serikali kwa njia ya mtandao na kushiriki katika kuinua uchumi wa kidijitali.

 

“Tumefanya kikao cha ndani na Watendaji Wakuu wa makampuni ya simu na kuongelea masuala ya vifurushi na bando, suala hili tunalifanyia kazi kwa pamoja na hivi karibuni Serikali itatoa tamko kuhusiana na masuala ya vifurushi”, amezungumza Ndugulile

 

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na watoa huduma za mawasiliano nchini kwa kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi na kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta ya mawasiliano.

 

Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Zainab Chaula alisema kuwa Serikali imewekeza katika TEHAMA ili kuwezesha na kuboresha uzalishaji na uendeshaji wa sekta takribani zote nchini, na kuwataka wadau wa sekta ya mawasiliano kutembea pamoja ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuipeleka nchi katika mapinduzi ya nne ya viwanda na uchumi wa kidijitali.

 

Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema Mfuko huo umeratibu kikao hicho cha wadau wa mawasiliano ikiwa ni agizo la Mhe. Waziri, ambapo moja ya ajenda ni kufanya majadiliano ya namna bora ya kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mipakani kwa kutumia teknolojia bora na rahisi.