Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI KUNDO- SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI


Na Immaculate Makilika – MAELEZO, DAR
 
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma kwa wananchi sambamba na kukuza uchumi wa nchi.
 
Amesema hayo jana wakati alipotembelea Kituo cha Kuhifadhi Data cha Wingu Afrika kilichopo jijini Dar es Salaam.
 
 
“Ninawashukuru kwa kuja kuwekeza hapa nchini kwa thamani ya takribani shilingi bilioni 17 hii ni dalili tosha kwamba tayari uwekezaji Tanzania katika mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano umeboreka sana, pia inatokana na faida kubwa ya kuwa na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022 ambayo inasaidia kuvutia wawekezaji wengi na kuwa na amani ya kuwekeza nchini,” ameeleza Naibu Waziri Kundo.
 
 
Aidha, amefafanua kuwa sera za nchi zinatoa fursa ya kuhakikisha kuwa sekta binafsi inashirikiana na Serikali ili kutengeneza fursa mbalimbali na hivyo uwepo wa Kituo hicho cha Kuhifadhi Data cha Wingu Afrika kunasaidia kutoa huduma katika nchi ambazo hazizungukwi na bahari mfano Zambia, Rwanda na Burundi.
 
 
“Uwepo wa Kituo hiki ambacho hakifungamani na upande wowote kimaslahi kutasaidia kutunza taarifa mbalimbali ikiwemo za kibenki hivyo kunaleta amani kwa nchi hizo kutumia huduma hii. Pia, kwa eneo hili ambalo nchi yetu ipo, uwepo wa vituo hivi vya kuhifadhi data unasaidia hata kuvutia makampuni makubwa duniani kama Amazon ili kuja kufanyakazi na sisi” Amesisitiza.
 
Naibu Waziri Kundo ameongeza kuwa Serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na sekta binafsi na tayari Shirika la Posta Tanzania (TTCL) limeshafika katika eneo hilo kwa ajili ya kutoa huduma hivyo kituo hicho kitafungua nchi kiuchumi na kusadia kuleta fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira kwa watanzania.
 
Kwa upande wake, Afisa Mikakati Mkuu wa Kituo cha Kuhifadhi Data ya Wingu Afrika, Bw. Nicholas Lodge ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini.
 
“Tunapata ujasiri wa kuwekeza Tanzania kwa kuwa kuna usalama wa mali na fedha zetu, hivyo tunaomba muendeelee kufanya hivyo ili kuvutia uwekezaji wengi zaidi pia huduma ziweze kupatikana kwa wingi zaidi kutoka katika mataifa mbalimbali,” amesema Bw. Lodge.
 
Naye, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Bw. Huneid Hussein Alli amesema kuwa wakezaji wameendelea kutoka nje ya nchi na kuja kuwekeza fedha nyingi nchini kwa kuwa kuna soko la uhakika na hivyo inasaidia kuitambulisha nchi kimataifa.