Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI MHANDISI KUNDO ATOA WITO KWA BARAZA LA WAFANYAKAZI


Wito umetolewa kwa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa kuzingatia vigezo walivyojiwekea.

 

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo  Mhandisi Kundo Mathew wakati akifungua Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo jijini Dodoma,ambapo amesema ili kutekeleza malengo ya wizara hiyo , ushirikiano wa hali ya juu unahitajika miongoni mwa viongozi wa wizara, watumishi  na wadau wa sekta ya mawasiliano kwa ujumla.

 

Aidha,Menejimenti ya wizara hiyo imetakiwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri na wezeshi ya utendaji kazi,mahusiano bora kazini pamoja na wafanyakazi kupata stahiki zao kwa muda muafaka na pale inaposhindikana taarifa sahihi zitolewe  kwa wakati husika.

 

Aliongeza kuwa,  kila mtumishi anatakiwa kusoma na kuelewa sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

 

“Kazi ya baraza la wafanyakazi ni kuangalia haki za wafanyakazi na utekelezaji wa wajibu wao, kwasababu haki na wajibu vinaenda sambamba”, Mhandisi Kundo

 

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula amesema kuna mafanikio yako mengi kupitia baraza hilo hasa katika kujenga nidhamu na utendaji wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

 

 Aliongeza kuwa , mkutano huo unajadili utekelezaji wa majukumu na mipango ya Wizara kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021, mapendekezo ya muundo mpya wa Wizara, kukumbushana kuhusu ujazaji wa fomu za kupima utendaji kazi (OPRAS) na kupokea taarifa za wafanyakazi kupitia wawakilishi wao

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi amesema wanania ya dhati ya kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari inakuwa mfano katika utendaji kazi kupitia umoja na mshikamano uliopo kama nguzo muhimu ya kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta mafanikio makubwa kwa sekta na taifa kwa ujumla.

 

Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Mawasiliano  na Teknolojia ya  Habari, Laurencia Masigo amesema wao kama TUGHE watahakikisha wanahamasisha ushirikiano katika kufanya kazi kwa kujituma ili kutumiza malengo ambayo wizara hiyo imejiwekea.

 

Hata hivyo, Wajumbe wa Baraza hilo wamekumbushwa majukumu ya Baraza la wafanyakazi mahali pa kazi kuwa ni pamoja na kuwashirikisha wafanyakazi wote katika utekelezaji wa shughuli za wizara kwa ushirikiano na menejimenti lakini pia kuishauri wizara juu ya mambo muhimu yanayohusu maslahi na hali bora ya wafanyakazi.